Jun 20, 2023 08:05 UTC
  • Wafadhili waahidi kutoa msaada wa dola bilioni 1.5 kwa ajili ya Sudan

Wafadhili wameahidi katika Mkutano wa Geneva wa Kukabiliana na Mgogoro wa Sudan, kutoa msaada wa kibinadamu wa takriban dola bilioni 1.5, wakati huu ambapo hali ya utulivu imetanda kwa kiasi fulani nchini Sudan kwa siku ya pili kutokana na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa baina ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Mwishoni mwa mkutano huo uliofanyika jana huko Geneva, Martin Griffiths, Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu alitangaza matokeo ya ahadi za kifedha zitakazotolewa ili kupunguza matatizo ya binadamu nchini Sudan na nchi jirani ambazo zinahifadhi wakimbizi wanaokimbia mapigano.

Akihutubia mkutano huo kwa njia ya video, Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdul Rahman Al Thani, alizitaka pande mbili zinazohusika katika mzozo wa Sudan kusitisha mapigano mara moja, na amepongeza juhudi za kimataifa za upatanishi za kujaribu kutatua mgogoro wa Sudan.

Waziri Mkuu wa Qatar ametangaza kuwa nchi yake inaahidi dola milioni 50 kusaidia mpango wa kukabiliana na dharura nchini Sudan, akibainisha kuwa Qatar imewasilisha tani 118 za chakula na dawa nchini Sudan tangu kuzuka kwa mzozo wa ndani kupitia daraja la anga.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry ametangaza kuwa nchi yake imeanzisha mpango wa pamoja na serikali ya Qatar kuhusu misaada ya kibinadamu nchini Sudan.

Shoukry amesisitiza haja ya kufikiwa usitishaji vita wa kudumu ili kusimamisha umwagaji damu wa watu wa Sudan, akibainisha kuwa Misri imepokea robo milioni ya Wasudan waliokimbia vita.

Saudi Arabia pia imeahidi kutoa msaada wa dola milionii 100 kwa ajili ya Sudan.

Katika hotuba yake wakati wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alielezea wasiwasi wake kuhusu kulengwa wafanyakazi wa huduma za misaada ya kibinadamu, akitoa wito kwa pande zinazohusika na mzozo na serikali za nchi jirani na Sudan kuwalinda raia na kuwezesha kazi za mashirika ya kibinadamu.

Guterres ameitaja hali ya Sudan kuwa ya kutia wasiwasi sana, akielezea kuwa ni vigumu kwa taasisi za misaada ya kibinadamu kufanya kazi katika mazingira ya sasa nchini Sudan.

Wizara ya Afya ya Sudan imetangaza kuwa, idadi ya watu waliouawa katika mapigano ya ndani nchini humo ni zaidi ya elfu tatu.

Tags