Ethiopia kuzindua awamu ya nne ya ujazaji maji katika bwawa lenye mvutano
Ethiopia inajiandaa kuanzisha awamu ya nne ya kujaza maji katika hifadhi ya bwawa lake kubwa katika Blue Nile. Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo licha ya upinzani wa jirani yake Misri.
Bwawa kubwa kwa jina la Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) lenye thamani ya dola bilioni 4.2 limekuwa kitovu cha mzozo wa kikanda tangu Ethiopia ilipojikita katika mradi huo mwaka 2011. Misri na wakati fulani Sudan kwa mara kadhaa zilikariri wito wao kwa serikali ya Addis Ababa wakiitaka isitishe zoezi la kujaza maji katika hifadhi ya bwawa hilo.
Demeke Mekonnen Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ameeleza kuwa, bwawa hilo sasa linakaribia marhala ya nne ya ujazaji maji na kwamba awamu tatu za kulijaza maji bwawa hilo haijayaathiri maeneo ya chini ya mto; vivyo hivyo awamu zilisosalia pia hazitakuwa na athari.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano kuhusu mto Nile huko Addis Ababa, Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema: Mradi wa bwawa kuu la Reinassance unakaribia kukamilika. Mkutano huo umejumuisha majadiliano ya ngazi ya juu ya mawaziri ambapo Demeke na Mawaziri wenzake wa Mambo ya Nje kutoka nchi za mto Nile kama Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan Kusini na Tanzania walishiriki pia. Hata hivyo si Sudan wala Misri ambazo ziko chini ya bwawa hilo la Ethiopia ambazo zilituma wawakilishi wao katika mkutano huo.
Itakumbukwa kuwa, Khartoumna Cairo zimesema mara kadhaa kwamba bwawa hilo kubwa linalojengwa na Ethiopia ni tishio kutokana na nchi hizo kutegemea maji kutoka mto Nile huku Ethiopia ikilitaja bwawa hilo kuwa muhimu kwake kwa ajili ya kutoa huduma ya umeme na maendeleo. Huku msimamo wa Khartoum ukionekana kubadilika, Misri ambayo inategemea mto Nile kwa asilimia 97 ya mahitaji ya umwagiliaji nchini inasisitiza kuwa bwawa kuu la Reinassance la Ethiopia ni tishio.
Kiongozi wa kijeshi wa Sudan Jenerali Abdel Fattah al Burhan mwezi Januari mwaka huu alisema kuwa Khartoum na Addis Ababa ziko pamoja na zimekubaliana kuhusu bwawa hilo.