Ethiopia yatuma maombi ya kujiunga na BRICS
(last modified Sat, 01 Jul 2023 04:46:37 GMT )
Jul 01, 2023 04:46 UTC
  • Ethiopia yatuma maombi ya kujiunga na BRICS

Ethiopia, ambayo ni miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika imeomba kujiunga na jumuiya ya BRICS ya chumi zinazoinukia. Haya yameelezwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.

Meles Alem, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia amesema kuwa wanataraji kuwa kundi la BRICS litatoa jibu chanya kwa ombi hilo. Alem ameongeza kuwa, Ethiopia itaendelea kufanya kazi na kushirikiana na taasisi za kimataifa ambazo zitalinda na kutetea maslahi yake.

Nchi hiyo ya pembe ya Afrika ni ya pili yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika huku uchumi wake ukishika nafasi ya 59 duniani kwa mujibu wa Mfuko wa Fedha Kimataifa (IMF). Mwaka jana Argentina ambayo inashika nafasi ya 23 duniani kwa upande wa uchumi ilisema kuwa China imeunga mkono ombi la nchi hiyo la kutaka kujiunga na kundi la BRICS.

BRICS ni jina la kundi linaloongozwa na mataifa yanayoinukia kiuchumi, ambalo linaundwa na nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. 

Mchakato wa maendeleo ya kiuchumi na kiviwanda wa wanachama wa BRICS unaonyesha kuwa harakati na fikra za kundi hilo zimejengeka katika msingi wa kuwa na nafasi muhimu katika ulimwengu ujao wa kambi kadhaa, jambo linalotambuliwa na mfumo unaotawala sasa duniani kuwa tishio kubwa kwake. 

Kundi la BRICS linaonekana kama kundi mbadala lenye nguvu linaloibukia lenye uwezo wa kuchuana na nchi za Magharibi kwa upande wa masoko. 

Hadi sasa nchi kadhaa zimewasilisha maombi kwa ajili ya kujiunga na kundi hilo. Kundi hilo aidha linaunda zaidi ya asilimia 40 ya idadi ya watu duniani huku likiwakilisha dunia kwa uchumi usiopungua asilimia 26. 

Afrika Kusini itakuwa mwenyeji wa mkutano ujao wa BRICS uliopangwa kufanyika mwezi Agosti.