Watu 8 wakiwemo watoto 6 wauawa katika mripuko wa bomu Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i99748-watu_8_wakiwemo_watoto_6_wauawa_katika_mripuko_wa_bomu_somalia
Watu wasiopungua wanane wakiwemo watoto sita wameuawa katika mripuko wa bomu uliotokea katika mji wa Bulaburde, jimboni Hirshabelle katikati ya Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2023 08:52 UTC
  • Watu 8 wakiwemo watoto 6 wauawa katika mripuko wa bomu Somalia

Watu wasiopungua wanane wakiwemo watoto sita wameuawa katika mripuko wa bomu uliotokea katika mji wa Bulaburde, jimboni Hirshabelle katikati ya Somalia.

Duru za habari zinaarifu kuwa, watu hao wameaga dunia leo Jumapili baada ya gari walililokuwa wakisafiria kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika kijiji cha Jicibow, yapata kilomita 220 kutoka Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.

Ibrahim Abdi Ali, afisa usalama katika mji wa Jowhar, makao makuu ya eneo la Hirshabelle katikati ya Somalia amesema waliopoteza maisha katika mripuko huo wa leo ni watu wa familia moja akthari yao wakiwa watoto wadogo.

Amesema hakuna shaka bomu hilo lilitegwa ardhini na wanamgambo wa al-Shabaab, na kwamba vyombo vya usalama vitawafuatilia na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa jinai hiyo. Hata hivyo kundi hilo la kigaidi halijatangaza kuhusika na shambulio hilo.

Wanachama wa al-Shabaab

Mripuko huo umejiri siku moja baada ya jeshi la Somalia na kikosi mpito cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (ATMIS) kutekeleza mashambulizi ya anga na ardhini kusini mwa Somalia na kuwaangamiza magaidi 40 wa kundi la al-Shabaab.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaida limekuwa likifanya kila liwezalo kuipindua serikali kuu ya Somalia tangu mwaka 2007; na hadi kufikia sasa kundi hilo limefanya mashambulizi mengi ya kigaidi na kuuwa wanajeshi na raia wengi.