Sep 07, 2024 02:49 UTC
  • Wanaharakati watoa mwito wa kukomeshwa mauaji dhidi ya wanawake Kenya

Makundi ya wanawake nchini Kenya yametoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia na mauaji dhidi ya wanawake katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Mwito huo umetolewa baada ya kifo cha mwanariadha mwingine ambaye aliuawa na mpenzi wake. Mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegei ambaye hivi karibunii alishiriki michezo ya Olimpiki inayoendelea Paris Ufaransa alifariki dunia siku ya Alkhamisi, siku nne baada ya mpenzi wake kummwagia petroli na kumchoma nyumbani kwake magharibi mwa Kenya. Mwanariadha huyo ni wa tatu wa kike kuuawa nchini Kenya tangu mwaka 2021.

Mwanzilishi wa shirika la Usikimye linalopambana na ukatili wa kijinsia Njeri Migwi amesema ukatili mwingi wa kijinsia hauchukuliwi kuwa ni uhalifu na hivyo kuitaka serikali kuchukua hatua. Takwimu za idadi ya wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia nchini Kenya zinatofautiana sana, ambazo wanaharakati wanasema hufunika ukubwa halisi wa tatizo.

 

Mwaka 2022, wanawake 725 walikufa nchini Kenya katika mauaji yanayohusiana na ukatili wa kijinsia, hiyo ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu mwaka 2015. Takwimu hizo zilikusanywa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa na Uhalifu.

Mauaji ya Cheptegei yanafuatia mauaji ya wanariadha wengine wawili maarufu wa Kenya. Mnamo Oktoba 2021, mwanariadha Mkenya aliyevunja rekodi Agnes Tirop, 25, aliuawa kwa kuchomwa kisu nyumbani kwake huko Iten. Mumewe aliyeachana naye alifikishwa mahakamani akituhumiwa kuhusika na mauaji yake na amekana mashtaka.  Aidha mnamo Aprili 2022, mwanariadha mwingine mzaliwa wa Kenya raia wa Bahrain Damaris Mutua alipatikana amekufa huko Iten Kenya katika tukio linaloshukiwa kuwa la unyanyasaji wa nyumbani.

Tags