Spoti, Oktoba 14
(last modified 2024-10-14T07:21:09+00:00 )
Oct 14, 2024 07:21 UTC
  • Spoti, Oktoba 14

Hujambo msikilizaji mpendwa na hususan ashiki wa habari na za spoti. Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa….

Wanakarate wa kike wa Iran wang'ara Italia

Wanakarate wa kike wa Iran, Fatemeh-Zahra Saeedabadi na Yalda Naghi-Beiranvand wameshinda medali za dhahabu na shaba mtawalia katika Mashindano ya 13 ya Dunia ya Karate yaliyoandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Karate (WKF) kwa Vijana na Mabarobao, huko Venice, Italia.

Mabinti wa Iran wang'ara upigaji makasia

Mbali na hayo, Zeinab Norouzi aliishindia Iran medali ya dhahabu katika Mashindano ya Upigaji Makasia ya 2024 ya Asia Jumamosi. Alivuka utepe wa ushindi kwa kutumia muda wa dakika 8, sekunde 02.721 katika mtindo wa sculls nyepesi. Kwa ujumla Iran imeshinda medali 2 za dhahabu, 3 za fedha na moja ya shaba kwenye mashindano hayo yaliyofanyika mjini Samarkand, Uzbekistan kuanzia Oktoba 10 hadi 14.

Kwengineko, klabu ya kandanda ya Bam Khatoon ya Iran imefuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya Asia baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 ilipochuana na College of Asian Scholars ya Thailand katika mchezo wao wa mwisho wa Kundi B Jumamosi. Ushindi huo umeifanya timu hiyo majanajike wa Iran kutuama katika nafasi ya pili kundini, nyuma ya Melbourne City FC ya Australia.

Mbali na hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ametoa ujumbe wa pongezi kwa timu za wasichana na wavulana za Iran kwa kung'ara katika mashindano ya dunia ya Taekwondo ya mwaka 2024 huko Chuncheon, Korea Kusini. Aidha Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amezipongeza timu hizo za Jamhuri ya Kiislamu kwa kuvuna ubingwa huo katika mashindano hayo ya dunia, ambapo ameshukuru juhudi zao pamoja na makocha na watendaji wote wa timu hizo.

Timu ya wasichana ya Iran ilipata medali nne za dhahabu na moja ya fedha, huku ya wavulana ikichota medali tatu za dhahabu, moja ya fedha na mbili za shaba katika mashindano hayo, yaliyofanyika Korea Kusini.

Mkenya avunja rekodi ya Chicago Marathon

Wanariadha wa Kenya John Korir na Ruth Chepngetich wameibuka washindi wa duru ya 46 ya Chicago Marathon nchini Marekani. Korir ametawala mbio hizo za kilomita 42 kwa upande wa wanaume kwa kutumia saa 2:02:43 akifuatwa kwa karibu na Muethiopia Mohamed Esa (2:04:39) na Mkenya Amos Kipruto (2:04:50).

Ruth Chepngetich

Dakika chache baadaye, bingwa wa dunia mwaka 2019 Ruth Chepngetich alinyakua taji lake la tatu la Chicago Marathon kwa rekodi mpya ya dunia ya saa 2:09:57. Chepngetich amefuta rekodi ya bingwa wa Berlin Marathon mwaka 2023, Tigst Assefa kutoka Ethiopia (2:11:53) kwa karibu dakika mbili. Chepngetich aliyemaliza makala ya 2023 nyuma ya Mholanzi Sifan Hassan, anakuwa mwanamke wa kwanza kabisa kukamilisha mbio hizo za kilomta 42 chini ya saa 2:10.

Soka Afrika

Timu ya taifa ya soka ya vijana wenye chini ya miaka 20 ya Tanzania 'Serengeti Boys' imefanikiwa kupata ushindi wa kishindo iliposhuka dimbani kuvaana na Rwanda katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON 2025. Serengeti ilivuna ushindi wa magoli 3-0 katika mchuano huo. Mabao ya mabarobaro hao wa Tanzania yalifungwa na Zidane Sereri dakika chache baada ya kupulizwa kipyenga cha kuanza ngoma, huku Sabri Kondo akifunga mawili katika dakika za 70 na 82 za mchezo.

Wakati huo huo, vijana wa Kenya "Rising Stars' waliwashukiwa vibaya wachovu Djibouti kwenye mchuano wa Jumapili, na kuwachabanga mabao 4-0. Katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam, Tanzania, vijana wa Kenya waliutandaza mpira na kucheza kiutu uzima, ambapo ushindi huo umewapaisha hadi kileleni mwa Kundi A kwa alama 7 kwenye mechi tatu walizocheza mpaka sasa. Stars watatinga nusu fainali iwapo watailima Sudan katika mchuano wa mwisho wa makundi utakaopigwa Jumanne katika Uwanja wa Azam Chamazi jiji Dar. Katika Kundi B, Uganda na Sudan Kusini zimeshajikatia tiketi za nusu fainali huku Burundi na Ethiopia zikitupwa nje ya mashindano hayo.

Na kwa kutatamatisha nikudokeza kwamba, Eritrea imeibuka kidedea kwenye Mashindano ya Uedesha Baiskeli ya Afrika huko Kenya, kwa kuzoa jumla ya medali 16, zikiwemo 7 za dhahabu. Afrika Kusini imeibuka ya pili huku Uganda ikifunga orodha ya tatu bora kwenye mashindano hayo ya siku 5 yaliyofanyika Iten, kauti ya Elgeto Marakwet, eneo la Bonde la Ufa.

……………..MWISHO…………

 

Tags