Hizbullah yawatwanga tena Wazayuni kwa zaidi ya makombora 100 + Video
Jeshi la utawala wa Kizayuni limekiri kwamba kwa uchache makombora 100 ya Hizbullah ya Lebanon yametwanga vituo vya kijeshi vya Israel katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Shirika la habari la Mehr limenukuu taarifa ya jeshi la utawala wa Kizayuni likikiri kwamba kwa uchache makombora 30 ya Hizbullah jana Jumapili yalipiga eneo la al Jalil pekee ambalo liko kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Kanali ya 12 ya televisheni ya Israel nayo imekiri kufanyika mashambulizi makubwa ya Hizbullah ikiwa ni pamoja na kwenye eneo la Tabaria.
Kwa upande wake Hizbullah ya Lebanon imesema katika taarifa yake leo Jumatatu kwamba, imeshambulia kambi tatu za kijeshi za utawala wa Kizayuni.
Harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu vile vile imesema kuwa, imewapiga kwa kombora wanajeshi wa Israel waliokuwa wamekusanyika kwenye kambi moja na kuwasambaratisha kabisa (kama inavyoonesha video iliyoambatana na habari hii).
Mashambulizi hayo ya Hizbullah ni majibu ya haki ya wanamapambano hao wa Kiislamu kutokana na jinai za kuchupa mipaka zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Lebanon na Ghaza, Palestina.
Vyombo vya habari vya Israel vimetangaza pia kwamba ving'ora vya hatari vimeendelea kusikika mfululizo katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambazo zimepichikwa jina bandia la Israel.