SEPAH: Magaidi 88 wameangamizwa na kutiwa mbaroni kusini mashariki mwa Iran + Video
Msemaji wa luteka ya kijeshi ya kambi ya Quds ya Jeshi la Nchi Kavu la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ametangaza habari ya kuangamizwa na kutiwa mbaroni magaidi 88 katika mazoezi ya kijeshi ya mashahidi wa usalama kwenye mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran.
Kwa mujibu wa IRIB, Kamanda Ahmad Shafaei alisema hayo jana na kuongeza kuwa, tangu kuanza luteka ya operesheni ya mashanidi wa usalama ya kambi ya Quds ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH hadi hivi sasa, magaidi 26 wameangamizwa, 50 wametiwa mbaroni na 12 wamejisalisha.
Amesema kuwa mazoezi hayo ya kijeshi yanaendelea na lengo lake kuu ni kupandisha kiwango wa utayari wa vikosi vya ulinzi sambamba na kuyasafisha magenge ya kigaidi kwenye maeneo hayo.
Msemaji wa mazoezi hayo ya kijeshi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) vilevile amesema kuwa, baada ya utawala wa Kizayuni kushindwa kukabiliana na kambi ya Muqawama huko Palestina na Lebanon umeamua kutumia magaidi kufanya vitendo vya kigaidi ndani ya Iran ambapo tarehe 26 Oktoba 2024, magaidi hao waliua shahidi na kidhulma maafisa kadhaa wa jeshi la polisi waliojitolea kwa ikhlasi na moyo mmoja kuilinda Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na watu wake. Lakini magaidi hao wamepata majibu makali na ya haraka na kwamba operesheni ya kusafisha magenge hayo ya kigaidi inaendelea kusini mashariki mwa Iran.