Ulimwengu wa Michezo, Jan 20
Karibu kwenye kipindi chako hiki kinachoangazia baadhi ya matukio makubwa na muhimu ya michezo kutoka kona mbali mbali za dunia ndani ya juma moja lililopita...
Iran ya 3 Kombe la Dunia la Kho Kho
Timu ya taifa ya wanaume ya Iran imefanikiwa kushika nafasi ya tatu katika duru ya uzinduzi wa Kombe la Dunia la Kho Kho, lililofanyika New Delhi, mji mkuu wa India. Timu ya Kho Kho ya Iran ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye michuano hiyo baada ya kushindwa na Nepal kwa alama 72-20 katika mpambano wa nusu fainali siku ya Jumapili. Iran imetunukiwa medali ya shaba kwa kuibuka mshindi wa tatu kwenye mashindano hayo ya kimataifa. Katika fainali, India iliisasambua Nepal 54-36 na kutwaa ubingwa. Hapo awali katika mashindano hayo, timu ya Iran ilipata ushindi dhidi ya Argentina (117-14), Afrika Kusini (56-32), na Ghana (61-30), na kutinga robo fainali. Katika robo fainali hiyo, Iran iliinyoa kwa chupa Kenya na kuizaba 86-18, na kuingia mzima mzima nusu fainali.

Toleo hili la kwanza la Kombe la Dunia la Kho Kho lilifanyika kwenye Uwanja wa Indira Gandhi huko New Delhi, kuanzia Januari 13 hadi 19. Kho Kho ni mchezo wa kitamaduni wa Asia Kusini wenye asili ya India na Nepal ya zamani. Ni mchezo wa pili maarufu wa kitamaduni huko India, baada ya kabaddi. Mchezo unachezwa kwenye uwanja wa mstatili na njia ya kati inayounganisha nguzo mbili ziko kwenye ncha zote mbili. Kho Kho, pamoja na michezo mingine ya kiasili ya India kama kabaddi na mallakhamb, ilionyeshwa pambizoni mwa Olimpiki ya Berlin mwaka 1936.
Soka: Sepahan bingwa Kombe la Super
Klabu ya soka ya Sepahan iliitandika Persepolis bao 1-0 na kushinda Kombe la Super la Iran kwa mara ya kwanza. Kiungo wa kati Mfaransa Steven Nzonzi alitikisa nyavu dakika mbili tu baada ya kuanza mechi hiyo kwenye Uwanja wa Imam Khomeini. Persepolis ilipata fursa kibao za kusawazisha, lakini wachezaji wake walikosa kutulia na kumakinika.

Super Cup hutunukiwa mshindi wa mechi kati ya bingwa wa msimu wa Ligi ya Ghuba ya Uajemi na mshindi wa Kombe la Hazfi (Mtoano).
Soka; Kombe Shirikisho Afrika; Simba Hoyee!
Klabu ya soka ya Simba ya Tanzania wikendi ilivuna ushindi wa aina yake kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam licha ya kutokuwa na mashabiki uwanjani. Msimbazi ilifungiwa na Shrikisho la Soka Afrika CAF kuingiza mashabiki kwa kosa lililotokea katika mchezo wao dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia.

Simba iliambulia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya CS Constantine ya Algeria, hapo kwa Mkapa. Ushindi huo umewafanya Wekundu wa Msimbazi wamalize mechi za makundi wakiwa kinara wa Kundi A, wakiizidi ujanja Constantine iliyosalia na pointi 12, huku Bravos do Maquis ya Angola iliyofumuliwa mabao 4-0 na CS Sfaxien ya Tunisia ikibaki ya tatu na pointi saba. Sfaxien ambayo ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 2004 baada ya kuunganishwa kwa michuano ya Kombe la Washindi na lile la CAF, inavuta mkia ikiwa na pointi tatu. Simba ililazimika kusubiri hadi kipindi cha pili kuweza kuandika mabao hayo, baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika bila timu yoyote kupata bao. Simba iliandika bao la kwanza dakika ya 61 lililofungwa na Kibu Denis aliyemalizia pasi safi ya nyota mpya wa kikosi hicho, Ellie Mpanzu aliyemgongea vizuri kabla ya mfungaji kufumua shuti kali lililomshinda nguvu kipa wa Constantine, Zakaria Bouhalfaya. Baada ya bao hilo wageni walifanya mabadiliko mengine ya wachezaji watatu, lakini ikawa ni kama mwiba kwao kwani walijikuta wakifungwa bao jingine la pili lililotiwa kimiani na Leonel Ateba dakika ya 79 akimalizia krosi ya chini ya beki wa kulia Shomari Kapombe. Matokeo hayo yameifanya Simba kulipiza kisasi cha kipigo ilichopewa katika mchezo wa kwanza dhidi ya Constantine walipowafumua mabao 2-1 mjini Constantine, Algeria, lakini imeiwezesha sasa kuwa na hakika ya kutokutana na vigogo watatu wa michuano hiyo, mabingwa watetezi Zamalek ya Misri, USM Alger ya Algeria au RS Berkane ya Morocco ambao nao wamemaliza kama vinara wa makundi yao ya B, C na D, kwa usanjari huo.

Wakati huo huo, klabu ya Yanga imeshindwa kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kulazimishwa sare tasa na MC Alger kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Matokeo hayo yameifanya Yanga imalize katika nafasi ya tatu kwenye kundi A ikiwa na pointi nane nyuma ya vinara Al Hilal yenye pointi 10 na MC Alger yenye pointi tisa katika nafasi ya pili.
Kwa kushindwa kutinga robo fainali, Yanga inakosa kiasi cha Dola 900,000 ambacho kila timu inayotinga hatua hiyo hutunukiwa na CAF. Yanga kwa kuishia hatua ya makundi, itaondoka na kifuta jasho cha Dola 700,000. Msimu uliopita, Yanga iliishia hatua ya robo fainali ambapo ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 3-2 na Mamelodi Sundownsya Afrika Kusini, baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare tasa.
Dondoo za Hapa na Pale
Klabu ya Al Hilal ya ligi kuu nchini Saudi Arabia imefuta jina la mshambuliaji wake mzawa wa Brazil, Neymar Jr kwenye mipango yao ya msimu huu ya kuwania taji la Saudi Pro League. Kocha wa Al Hilal Jorge Jesus alisema, ”Ney hatasajiliwa, lakini anaweza kushiriki Ligi ya Mabingwa ya Asia. Yeye ni mchezaji wa kiwango cha ulimwengu. Lakini kimwili, Neymar Jr hawezi tena kucheza kwa kiwango ambacho sisi sote tumezoea kuona. Bado yuko chini ya mkataba na Al Hilal na ataamua mwenye mustakabali wake”.

Kwengineko, licha ya mkufunzi Mikel Arteta kuionya Liverpool kuwa Arsenal wamerejea kwenye vita vya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, baada ya kuonyesha umahiri wakiwalemea majirani Tottenham Hotspur kwa kuwazaba mabao 2-1 ugani Emirates Jumatano ya Januari 15, lakini wikendi walijikuta tena wakiboronga. Wabeba Bunduki walihitaji ushindi huo sana ili kupunguza mwanya kati yao na vinara Liverpool. Baada ya ushindi wa Jumatano, kilichofuata wikendi ni kulazimishwa sare ya mabao 2-2 waliposhuka dimbani kuvaana na Aston Villa. Arsenal sasa wana alama 44, pointi sita nyumba na mibabe Liverpool wenye alama 50. Watani wa Gunners, klabu ya Manchester United United siku ya Jumapili walizamishwa na Brighton na kukubali kichapo chema cha mabao 3-1. Aidha Jumamosi, Liverpool ilimnyoa Brentford mabao 2-0, katika Uwanja wa GTech Community, jijini London. Mabao hayo ya Liverpool walioko kileleni mwa jedwali la EPL yalifungwa na Darwin Nunez katika dakika za majeraha.
Na klabu ya Shabab Al Ahli imefanikiwa kutwaa taji lake la pili mfululizo la Qatar-UAE Super Cup, kwa kuwalaza wenyeji Al Rayyan mabao 3-1 na kunyanyua Ngao ya Challenge kwenye Uwanja wa Ahmad Bin Ali. Mabao ya Shabab Al Ahli yalitokana na buti za Yuri César (dakika ya 28), Muirani Sardar Azmoun (dakika ya 52) na Guilherme Bala katika dakika za nyongeza.
……………..MWISHO………….