Spoti, Mei 5
(last modified Mon, 05 May 2025 07:17:58 GMT )
May 05, 2025 07:17 UTC
  • Spoti, Mei 5

Karibu tuangazie japo kwa mukhtasari baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri katika muda wa juma moja lililopita kote duniani.

Teractor yatwaa Ligi ya Soka ya Iran

Klabu ya soka ya Teraktor Sazi imetwaa ubingwa wa Ligi ya Wataalamu ya Ghuba ya Uajemi (PGPL) kwa mara ya kwanza katika historia yake. Klabu hiyo ya soka yenye makao yake mjini Tabriz iliigaragaza Shams Azar mabao 4-0 mjini Qazvin na kushinda taji hilo, zikiwa zimesalia wiki mbili kabla ya ligi kumalizika rasmi. Domagoj Drozdek alifanikiwa kucheka na nyavu mara mbili, huku mabao ya Amirhossein Hosseinzadeh na Ricardo Alves yakilizamisha kabisa jahazi la Shams Azar. Beki wa kati wa Shams Hooman Rabizadeh alilishwa kadi nyekundu kunako dakika ya 83 ya mchezo.

Wachezaji wa Teractor wakiwa dimbani

 

Siku ya Ijumaa, wakazi wa mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran, ambako ni makao makuu ya watengeneza matrekta wa Iran, walijitokeza mitaani kwa mbwembwe, vifijo na hoi kusherehekea ushindi huo.

Mjini Isfahan, katikati mwa Iran, klabu ya Sepahan ambayo ipo katika afasi ya pili jedwalini kwa alama 56, ilikubali kuzabwa na Gol Gohar mabao 2-1. Amirmohammad Razaghinia na Mehdi Tikdari walifanikiwa kutikisa nyavu za wageni. Beki wa Sepahan, Arya Yousefi alipigwa kadi nyekundu kweye mchuano huo kabla ya mapumziko. Mohammadmehdi Mohebbi alipunguza nakisi ya mabao kwa bao lake la dakika ya 75. Nayo klabu ya Persepolis iliishinda Mes mabao 3-0 kwenye mchuano mwingine wa karibuni wa Ligi Kuu ya Soka ya Iran. Katika mechi hiyo iliyopigwa Rafsanjan siku ya Alkhamisi, Ali Alipour alifunga mabao 2, huku bao la Serdar Dursun likizima kabisa matumaini ya Mes. Persepolis imesalia katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 54, pointi saba nyuma ya viongozi Teractor. Katika hatua nyingine, timu ya Esteghlal iliwazaba watengeneza Alumini mabao 5-1 mjini Tehran, shukrani kwa mabao ya Ramin Rezaeian, Mohammadhossein Eslami, Masoud Joma na Joel Kojo (mabao mawili).

Malavan pia walipambana kiume na kutoa sare ya kufungana mabao 3-3 huko Bandar Anzali.  ُSi vibaya kuashiria hapa kuwa, klabu ya soka ya Persepolis inasalia kuwa moto wa kuotea mbali, kwani imeshinda taji hilo mara tisa kati ya duru 24 za mashindano hayo, ikifuatiwa na Sepahan yenye mataji matano.

Soka ya Ufukweni; Iran yaanza vizuri

Iran imeanza vizuri mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA la Soka ya Ufukweni ya Ushelisheli 2025. Hii ni baada ya kushinda mechi zake za ufunguzi, ikiwemo mechi ya Jumamosi dhidi ya Paraguay. Safu dhaifu ya ulinzi ya Paraguay iliibeba Iran na kuipelekea ipate ushindi wa pili mfululizo katika Mashindano ya Soka ya Ufukweni ya Dunia ya Ushelisheli 2025. Iran iliigaragaza Paraguay mabao 5-1 katika mashindano hayo ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA. Iran ilianza kwa kasi huku Movahed Mohammadpour na Mehdi Mirjalili kila mmoja akifunga bao kupitia mikwaju ya mbali. Majaribio ya Paraguay kupunguza nakisi ya mabao yalitatizwa hadi katikati ya kipindi cha pili, wakati Milciades Medina aliporuka na kufunga bao la kustaajabisha la baiskeli. Ali Nazem aliifungia Iran jingine, likifuatiwa na kombora jingine la Mahdi Shirmohammadi, huku Mohammad Masoumi akiifungia Timu Melli ya Iran bao la tano.

Iran yapania kutinga fainali

 

Kabla ya hapo, Iran iliitandika Mauritania mabao 5-4 katika mchuano mwingine wa Kundi B ya siku ya Alkhamisi. Iran ilinusurika pambano hilo kali kutoka kwa Mauritania baada ya vijana hao wa Ali Naderi kufunga mabao manne katika kipindi cha kwanza huku hat-trick ya Cheikh Belkheir nusra ipeleke mechi hiyo katika muda wa ziada. Mashindano hayo ya dunia yaliyoanza Mei Mosi, yatamalizika Mei 11.

Kombe la Muungano; Ni Yanga na JKU fainali

Klabu ya Yanga ya Tanzania imefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Muungano 2025 baada ya kuibwaga Zimamoto FC ya Zanzibar kwenye mikwaju ya penalty, kwa kuitibua mabao 3-1, kufuatia sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za kawaida. Yanga SC walitangulia kwa bao kupitia kwa Maxi Nzengeli dakika ya 29, huku Zimamoto wakisawazisha kupitia Said Mwinyi kunako dakika ya 71. Baada ya muda wa kawaida kumalizika kwa sare, mshindi aliamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambapo Zimamoto FC walikosa penalti tatu kati ya nne walizopiga, huku Yanga SC wakifunga penalti tatu kati ya nne walizopiga.

 

Kwa matokeo hayo, Yanga SC sasa watakutana na JKU FC ya Zanzibar kwenye fainali ya kusisimua ya Kombe la Muungano 2025.

Huku hayo yakiarifiwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 15 kwa kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Mpira wa Miguu kwa Shule za Afrika (CAF African Schools Football Championship) kwa mara ya pili mfululizo. Amesema, “Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 15 ya Tanzania, nawapongeza kwa ushindi wenu wa kihistoria. Ninajivunia mafanikio yenu kwani ni fahari kwa Taifa letu na ni chachu ya maendeleo ya sekta ya michezo hapa nchini.” Aidha, Rais Samia ameipongeza Timu ya Taifa ya Wanawake ya Futsal kwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya Mashindano ya Mataifa ya Afrika (Women’s Futsal Cup of Nations 2025).

Wakati huo huo, Rais William Ruto amesisitiza kujitolea kwa serikali yake kukuza vipaji vya michezo nchini Kenya. Alizungumza hayo katika Ikulu ya Nairobi, siku ya Ijumaa, wakati wa mapokezi ya Kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA Champions League). Rais Ruto alisema serikali, kwa ushirikiano na washikadau wengine, itaendelea kuwekeza rasilimali za kutosha katika kukuza vipaji vya soka na kufufua miundo msingi ya soka.

Soka na Palestina Kenya

Moyo wa mshikamano na michezo ulionekana karibuni katika ufukwe wa Mombasa, pale Pwani ya Kenya ilipoandaa Kombe la Uhuru wa Palestina, mashindano ya kandanda ya wachezaji 7 kila upande ambayo yalileta pamoja timu zenye shauku, na wafuasi wa malengo ya Palestina. Kwenye mashindao hayo yaliyofanyika karibuni katika Uwanja wa Michezo wa Serani, Mbaraki, huko Mombasa, timu za wenyeji zilijipinda zikiwania si tu kombe, bali pia kuhamasisha na kuongeza ufahamu wa kadhia ya Palestina, sanjari na kuonyesha upinzani dhidi ya jinai za Israel kupitia michezo. Baada ya msururu wa raundi kali za mtoano, klabu ya Mombasa Phoenix iliibuka kidedea, na kuwatoa Muslim Brothers katika mchuano wa fainali uliokuwa na ushindani mkali.  "Nishati uwanjani ilikuwa ya ajabu," mmoja wa waandaaji wa mashindano hayo alisema na kuongeza kuwa, “Vijana hawa walicheza kwa moyo—si kwa ajili ya ushindi tu, bali kwa ajili ya haki.” Bendera na mabango ya Wapalestina yanayotaka uhuru na haki yalijaa ukumbini, na hafla fupi ya kuonyesha mshikamano na Wapalestina ilifanyika kabla ya mechi ya fainali.

 

Vibanda vya elimu viliangazia mzozo wa kibinadamu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. "Hii ni zaidi ya soka," alisema mchezaji kutoka Muslim Brothers. "Ni njia yetu ya kusema, 'Tunasimama na Palestina. Na tunakataa ubaguzi wa rangi, uvamizi na ukandamizaji." Mipango tayari inaendelea kufanya Kombe la Uhuru wa Palestina kuwa tukio la kila mwaka la mchezo. Tuzo zilitolewa na Abdulqadir A. Nasser, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mshikamano ya Kenya na Palestina [Kenya Palestine Solidarity Movement (KPSM)]; Abdallah Ali Sheikh, mwanachama wa Tawi la Mombasa la Jumuiya ya Kenya na Palestina; na Abdulrazak Hassan Mohamed, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Al-Qaim.

Kombe la Wataalamu Asia; al-Ahly ya Saudia bingwa

Klabu ya Al Ahli ya Saudi Arabia iliiadhibu Kawasaki Frontale ya Japan mabao 2-0 katika mchezo wa fainali na kushinda mashindao ya kwanza ya Ligi ya Weledi wa Asia Jumamosi. Kikosi cha nyota cha Jeddah, kikicheza nyumbani mbele ya mashabiki 60,000 kwenye Uwanja wa King Abdullah Sports City, kilistahili ushindi huo mnono kwa kujitutumua na kukamilisha michuano hiyo bila kushindwa.

Chelsea mguu moja ndani fainali Ligi ya Confrence

Na klabu ya soka ya Chelsea inajongea fainali ya Confrence League, baada ya kuikung'uta Djurgaarden mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali ya ligi hiyo, licha ya kuupigia ugenini. Chelsea iitawala mchezo huo katika karibu kipindi chote, huku ikicheza soka la utu uzima kwenye mechi hiyo iliyopigwa katika Uwanja wa 3Arena. Timu mbili hizo zitavaana tena kwenye mechi ya marudiano mnamo Mei 8, ambapo The Blues wanatazamiwa kuteleza hadi fainali kiwepesi, kwani wataupigia mchano huo nyumbani Stamford Bridge. Mchezo wa fainali ya Conference League utafanyika Mei 28 mwaka huu nchini Poland katika Uwanja wa Wrocław.

……………..MWISHO………….