Ulimwengu wa Spoti, Mei 19
Hujambo msikilizaji mpenzi. Karibu tudondoe baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri katika kipindi cha wiki moja iliyopita kitaifa, kieneo na kimataifa.....
Sepahan yaiadhibu Esteghlal na kumaliza ya pili
Klabu ya soka ya Sepahan siku ya Alkhamisi iliichabanga Esteghlal mabao 3-1 na kumaliza ya pili kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Iran inayofahamika pia kama Ligi ya Wataalamu ya Ghuba ya Uajemi ya 2024/25 (PGPL). Mchezaji wa Esteghlal Mohammadhossein Eslami alifunga goli katika dakika ya 10, lakini Kaveh Rezaei alifanya kuwa sawa bin sawa kunako dakika ya 36. Mohammadmehdi Mohebbi alifanya matokeo kuwa 2-1 katika dakika ya 76 kalba ya Wissam Ben Yedder kuifungia Sepahan jingine la fungakazi. Sepehan imemaliza ya pili ikiwa na alama 60, zikiwa ni pointi 8 nyuma ya mibabe Teractor Sazi. Katika Uwanja wa Azadi mjini Tehran, Persepolis iliinyoa kwa chupa Havadar ambayo tayari imeshushwa daraja, kwa kuizaba mabaoa 2-0, shukrani kwa mabao mawili ya dakika za lala salama kutoka kwa Oston Urunov na Yaghoub Barajeh.

Wekundu wa Tehran ambao wamefikisha pia alama 60, wanamaliza ligi katika nafasi ya 3. Sepahan sasa imejiunga na Tractor, mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Iran; na inatazamiwa kuiwakilisha Iran katika mchujo wa Ligi ya Mabingwa wa Asia 2025/26. Ikumbukwe kuwa, wiki iliyopita, klabu ya soka ya Teraktor Sazi ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Iran kwa mara ya kwanza katika historia yake., baada ya kuigaragaza Shams Azar mabao 4-0 mjini Qazvin na kushinda taji hilo.
Handiboli ya Ufukweli; Iran mshindi wa 2
Iran ilishindwa kufurukuta mbele Oman na kukubali kulimwa 2-0 katika mechi ya fainali ya Mashindano ya 10 ya Mpira wa Mikono ya Ufukweni ya Asia yaliyofanyika Muscat, mji mkuu wa Oman. Hudhaifa Al-Siyabi alitajwa kuwa mchezaji bora wa mechi kwa uchezaji wake wa kipekee kwenye fainali hiyo. Zaidi ya hayo, Pakistan ilipata nafasi ya tatu baada ya kuishinda Jordan, huku kwa upande wa wanawake, Vietnam ilitwaa ubingwa, ikifuatiwa na Ufilipino katika nafasi ya pili, na India katika nafasi ya tatu. Iran na Oman zitaliwakilisha bara Asia katika Mashindano ya Dunia ya IHF Beach Handball.
Futsal ya Wanawake Asia; Japan yapindua meza ya Iran
Iran iliishinda China katika mchujo wa kuwania nafasi ya tatu ya Kombe la AFC la Wanawake la Futsal Asia China 2025 siku ya Jumamosi na kujihakikishia nafasi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA la Futsal litakalopigwa nchini Ufilipino baadaye mwaka huu 2025.

Mabingwa hao mara mbili walimaliza kampeni yao kwa kishindo mbele ya umati wa watu waliofurika katika Ukumbi wa Michezo wa Hohhot, huku ushindi wa mabao 3-1 ukihakikisha kwamba wataungana na Thailand na Japan kwenye fainali ya kwanza ya Kombe la Dunia itakayoanza Novemba. Maral Torkaman alifunga mabao mawili pamoja na bao la Nastaran Moghimi. Cao Jiayi alikuwa analenga China.
CAF U-20; Afrika Kusini Bingwa
Afrika Kusini ilishinda taji lao la kwanza la Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye chini ya miaka 20. Mabarobaro hao wa Afrika Kusini walishinda japo kwa mbinde, baada ya kuizaba Morocco bao 1-0 katika mchezo wa fainali wa TotalEnergies CAF U-20 Jumapili usiku katika Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo.

Bao la aina yake la Gomolemo Kekana lilipatikana katika dakika ya 70 baada ya mchezaji huyo kuachia shuti kali la mguu wa kulia kutoka nje ya eneo la hatari, na kuupinda mpira kwenye kona ya juu.
Riadha: Kenya yang'aa Diamond League
Rais William Ruto ameipongeza timu ya riadha ya Kenya kwa matokeo mazuri katika Ligi ya Almasi ya Doha 2025. Miongoni mwa washindi ni Reynold Cheruiyot, ambaye alishinda katika mbio za mita 5,000. Nelly Chepchirchir alishinda mbio za mita 1,500, huku Susan Lokayo Ejore akipata nafasi ya pili katika mashindano hayo hayo. Faith Cherotich alitwaa ushindi katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi. Wyclife Kinyamal alimaliza wa pili katika mbio za mita 800. Wakati huo huo, mwanariadha mwenye mbio zaidi wa Afrika, Ferdinand Omanyala kutoka Kenya amevunja rekodi yake mwenyewe ya Afrika katika mbio za mita 150, baada ya kukata utepe wa ushindi wa mbio hizo katika mashindano ya Adidas Atlanta City Jumamosi usiku huko Georgia nchini Marekani.

Omanyala kwa kutumia sekunde 14.70 aliwabwaga Terrence Jones wa Bahamas na Mathew Boling wa Marekani. Omanyala sasa anatazamiwa kushiriki mashindano yake ya tatu ya Diamond League msimu huu mjini Rabat, Morocco, Mei 25.
Yanga fainali Kombe la Shirikisho
Mabingwa watetezi wa CRDB Federation Cup, Yanga SC wametinga kibabe hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho. Katika mchezo wa nusu fainali michuano hiyo iliyopigwa Jumapili Mei 18, Wananchi walivuna ushindi kwa kuizaba JKT mabao 2-0 katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Mabao ya Prince Dube dakika ya 41 kwa makosa ya safu ya ulinzi ya JKT Tanzania akiwa ndani ya 18 na bao la pili limefungwa na Mudathir Yahya dakika ya 90 kwa pasi ya Clatous Chama. Yanga SC inatangulia fainali ikisubiri mshindi wa mchezo wa nusu fainali kati ya Simba SC dhidi ya Singida Black. Wababe hawa wawili Simba SC na Singida Black Stars wanatarajiwa kucheza Mei 31.
Wakati huo huo, klabu ya Simba inawajihiwa na kibarua cha kigumu katika mchezo wa mkondo wa pili wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) dhidi ya RS Berkane utakaopigwa Jumapili ya Mei 25. Hii ni baada ya Wekundu wa Msimbazi kukubali kulishwa kichapo na Waarabu hao Morocco katika mechi ya mkondo wa kwanza wa fainali hiyo ugenini usiku wa Jumanne ya Mei 17. Simba ilijikuta inaheheshwa katika dakika za mwanzo za mchezo, na kuishia kulimwa mawili hayo ndani ya dakika 15. Simba ilifanikiwa kutinga fainali licha ya kutoa sare tasa na Stellenboch FC ya Afrika Kusini katika mchuano wa ugenini kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, Durban, ikibebwa na ushindi iliopata wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza ya Aprili 20 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Wachezaji na wasimamizi wa Simba wanasisitiza kuwa, licha ya kucharazwa 2-0 na Barkane ya Morocco, lakini rekodi za kung'ara Wekundu wa Msimbazi katika mechi za marudiano hasa zinapopigwa nyumbani zinaipa matumaini klabu hiyo ya Tanzania.
Dondoo za Hapa na Pale
Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Michezo wa Palestina, ametangaza kuuawa shahidi kwa wanariadha 560 wa Kipalestina na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya michezo katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza hujuma ya kinyama ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023.

Muntaser Adkaydek, Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Michezo wa Palestina, amesema hayo katika katika Kongamano la AIPS huko Rabat, Morocco na kuongeza kuwa, kulenga wanariadha na miundombinu ya michezo kunatishia mustakabali wa michezo ya Palestina, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kukomesha mashambulizi haya.
Katika hatua nyingine, klabu ya soka ya Barcelona siku ya Alkhamisi ilitwaa taji lake la 28 la Ligi ya Uhispania baada ya Lamine Yamal kung'ara katika ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya hasimu Espanyol. Yamal alifunga dakika ya 53 ya mechi hiyo kali, kwa kutumia mguu wa kushoto na kutikisa kona ya nyavu.

Fermin Lopez alifunga dakika za lala salama na kuhitimisha ushindi huo, lakini ni bao la Yamal ambalo liliteka vichwa vya habari na kuwa kilele mwafaka kwa msimu wa chipukizi huyo.
Kwengineko, Eberechi Eze wa Crystal Palace aliamsha sherehe kubwa kusini mwa London kwa kufunga bao pekee na kushinda Kombe la FA dhidi ya Manchester City na kutwaa taji la kwanza kuu la klabu hiyo katika historia yao.
.....................MWISHO...............