Spoti, Juni 2
(last modified Mon, 02 Jun 2025 07:01:57 GMT )
Jun 02, 2025 07:01 UTC
  • Spoti, Juni 2

Hujamo mskilizaji mpenzi, natumai u bukheri wa afya. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu yayojiri viwanjani ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa…..nakusihi tuwe sote hadi tamati…karibu…..

Muirani aweka historia Korea Kusini

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amempongeza mwanamichezo wa Iran Reyhaneh Mobini Arani kwa ushindi wake wa kihistoria katika Mashindano ya Riadha ya Asia 2025. Katika ujumbe aliotuma kwenye akaunti yake ya X Ijumaa jioni, Dkt Pezeshkian alipongeza ubingwa wa Mobini katika mashindano ya kuruka ya wanawake kwenye mashindano yaliyofanyika Korea Kusini. Mafanikio hayo, amesema, sio tu ni medali ya kwanza ya dhahabu ya kihistoria aliyopata mwanamke wa Iran katika nyanja ya riadha, lakini pia ni alama ya azma isiyoyumba ya wanawake wa Iran ya kupata mafanikio katika uga wa kimataifa.

Reyhaneh Mobini

 

Mwanariadha huyo wa Iran katika mchezo wa kuruka, Reyhaneh Mobini alionyesha mchezo wa kufana katika siku ya tatu ya Mashindano ya 26 ya Riadha ya Asia nchini Korea Kusini, ambapo aliibuka kidedea na kutwaa medali dhahabu kwa kuruka umbali wa mita 6.40. Mshindani wake wa karibu zaidi, Sujan Edapilly wa India aliibuka wa pili kwa kuruka mita 6.33, huku orodha ya tatu bora ikifungwa na Shaili Singh wa India aliyeruka umbali wa mita 6.30. Ushindi wa Mobini, ambaye ni mwanachuo anayetaka kuwa daktari wa meno unaonyesha kuongezeka kwa uwepo wa Iran katika riadha ya wanawake kimataifa, na kuonyesha nguvu na usahihi katika uwanja wa ushindani mkali.

Mashindano ya Riadha ya Asia huwaleta pamoja wanariadha nyota kutoka bara lote, na kuweka mazingira kwa ajili ya mashindano yajayo ya Olimpiki na kimataifa. Aidha ushindi wa Mobini unaashiria mafanikio makubwa kwa michezo ya wanawake ya Iran katika ngazi ya kimataifa. Wakati huo huo, mwanamichezo wa Iran, MohammadrezaTayebi alitwaa dhahabu katika mchezo wa kurusha ufe, baada ya kulitupa umbali wa mita 20.32. Mchina Xing Jailiang alinyakua fedha na mita 19.97, na medali ya shaba ilienda kwa Mohammed Tolu kutoka Saudi Arabia naliyerusha mita 19.92.

Kombe la Hazfi; Esteghlal kidedea

Rouzbeh Cheshmi alifunga bao la dakika za mwisho katika ushindi wa Esteghlal dhidi ya Malavan katika mechi ya mwisho ya Kombe la Hazfi (Kombe la Mtoano) kwa msimu wa mwaka 2024/25. Katika mechi hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Imam Khomeini wa Arak, Cheshmi alifanikiwa kucheka na nyavu katika dakika ya 120 ya mchezo. 

Wachezaji wa Esteghlal wakishangilia bao

 

Malavan ilitinga fainali baada ya kuitandika Gol Gohar bao 1-0, wakati ambapo Esteghlal iliizaba Sanat Naft mabao 2-0 katika mchezo mwingine wa nusu fainali. Esteghlal na Malavan sasa zitaiwakilisha Iran katika Ligi ya Mabingwa ya Asia AFC 2025/26. Si vibaya kuashiria hapa kuwa, Esteqlal inasalia klabu yenye mafanikio zaidi katika historia ya Kombe la Hazfi, ikiwa imeshinda taji hilo mara nane sasa. Malavan wametwaa kombe hilo mara tatu.

Voliboli; Iran yang'ara

Timu ya voliboli ya Iran 'B' ilifuzu kwa raundi inayofuata ya Ligi ya Mataifa ya Wanaume ya CAVA ya 2025 kama washindi wa Kundi A. Iran ilianza kampeni yake kwa ushindi dhidi ya Turkmenistan 3-1 na kuendelea kushinda India 3-1 na Uzbekistan 3-0. Chini ya uongozi wa Peyman Akbari, timu hiyo imeratibiwa kumenyana na Kazakhstan na Pakistan siku ya Jumatatu na Jumanne, mtawalia. Mashindano hayo yaliyoanza Mei 29, yataendelea hadi Juni 4 huko Fergana, Uzbekistan. Awali, michuano hiyo ilipangwa kufanyika nchini Pakistani lakini ilibidi ihamishwe kutokana na mzozo wa Pakistan na India.

 

Wakati huo huo, timu ya taifa ya voliboli ya Iran iliishinda Italia 3-2 (23-25, 25-18, 14-25, 25-21, 15-11) katika mechi ya kirafiki siku ya Ijumaa. Hata hivyo, timu hiyo ya taifa ya voliboli ya wanaume ya Iran ilipokutana tena na Italia siku ya Jumamosi, iliamua kusalimu amri kwa kuzabwa seti 3-0 (25-22, 25-23, 25-19).  Michezo hii ya kirafiki ni sehemu ya maandalizi ya Iran kwa Ligi ya Mataifa ya Mpira wa Wavu (VNL) ya 2025. Timu ya Roberto Piazza itaanza kampeni ya kifahari dhidi ya Brazil mnamo Juni 11 huko Rio de Janeiro. Iran pia itashindana dhidi ya Marekani, Slovenia na Ukraine katika mechi zinazofuata katika Wiki ya 1.

Nani zaidi? Pyramids vs Mamelodi

Mechi ya marudiano baina ya klabu ya soka ya Pyramids ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ilisakatwa jijini Cairo Jumapili hii ya Juni 1. Pyramids hatimaye imetwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia, baada ya kuicharaza Mamelodi Sundowns magoli ya jumla ya 3-2 kwenye fainali hiyo. Sundowns ikilazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza katika dimba la Loftus Versfeld, Pretoria Afrika Kusini kabla ya kulazwa mabao 2-1 katika Dimba la Juni 30, huko Cairo, mji mkuu wa Misri, ukiwa ni mchezo wa marudiano. Wachezaji wawili raia wa Morocco, Walid El Karti na Mohamed Chibi wote walianza kwa Pyramids kwenye Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo. El Karti alicheza dakika zote 90, huku Chibi akitolewa dakika ya 88 baada ya kutoa pasi ya bao. Pyramids walianza kufunga dakika ya 23 kupitia kwa Mtanzania Fiston Mayele, na kuongoza kwa bao 1-0 hadi mapumziko. Waliongeza faida yao mapema katika kipindi cha pili pale Ahmed Samy alipounganisha krosi ya moja kwa moja kutoka kwa Chibi dakika ya 56. Sundowns walipata bao dakika ya 75 kupitia Iqraam Rayners, lakini halikutosha kuwazuia Pyramids kutwaa taji lao la kwanza la kibara.

Pyramids, moto wa kuotea mbali

 

Pyramids FC ilikuwa haijawahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati ambapo Mamelodi Sundowns imechukua ubingwa huo mara moja 2016. Mwamba, Fiston Mayele amepata kiatu cha pili cha dhahabu kwa ufungaji bora kwenye michuano hiyo ya CAF. Kiatu chake cha kwanza alikipata akiwa na Yanga SC ya Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) akimaliza na magoli saba msimu wa 2023. Lakini mwaka huu, Mayele ametwaa kiatu cha ufungaji bora cha Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) akiwa na Pyramids FC akimaliza michuano hiyo na magoli 6 huku akitwaa ubingwa wa CAF kwa mara ya kwanza.

Tanzia; wanariadha wasiopungua 21 wa Jimbo la Kano waliaga dunia siku ya Jumamosi basi lao lilipopoteza mwelekeo na kuanguka kutoka kwenye daraja katika Eneo la Serikali ya Mtaa la Kura walipokuwa wakirejea kutoka kwa Tamasha la Kitaifa la Michezo katika Jimbo la Ogun, kusini magharibi mwa Nigeria. Gari hilo lililokuwa limebeba abiria 35, wengi wao wakiwa wanariadha na maafisa, lilikuwa likirejea kutoka kwa tamasha la michezo wakati ajali mbaya ilipotokea kabla ya kufika wanakoenda, alisema afisa mmoja mkuu. Umar Faggie, mwenyekiti wa tume ya michezo ya jimbo hilo, aliiambia Anadolu kwa njia ya simu kwamba "wanariadha hao walikuwa wakisafiri kwa basi la Tume ya Michezo ya Jimbo la Kano wakati lilipopinduka kutoka kwenye daraja." Manusura wa ajali hiyo ya barabarani wamepelekwa hospitali kwa matibabu ya dharura.

Dondoo za Hapa na Pale

Klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa ndio mabingwa wa Ulaya baada ya kuinyoa kwa chupa, tena bila maji Inter Milan, kwa kuichabanga mabao 5-0 kwenye fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Ulaya. Hatimaye, klabu hiyo ambayo imebadilishwa na mabilioni ya dola ya Qatar, na kununua wachezaji wakubwa duniani, imetuama kileleni, na juhudi zake hizo hatimaye zimezaa matunda. Haukuwa tu ushindi wa kwanza wa PSG katika fainali ya tuzo kubwa zaidi ya klabu za soka za Ulaya, lakini tofauti ya ushindi katika mechi ya Munich pia ni rekodi ya aina yake ya fainali ya shindano hilo. Wametwaa taji ambalo hata Lionel Messi, Neymar Jr, Zlatan Ibrahimovic au Kylian Mbappe hawakuweza kulitwaa, na hatimaye ndoto ya klabu hiyo ya Ufaransa chini ya Luis Enrique, kocha wa Uhispania imetimia. Bao la kwanza la Achraf Hakimi katika dakika ya 12 dhidi ya klabu yake ya zamani, na mabao mawili kutoka kwa fowadi mwenye umri wa miaka 19 Désiré Doué -- ambaye alikua kijana wa kwanza kufunga mara mbili kwenye fainali tangu Eusebio wa Benfica katika ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Real Madrid mnamo 1962 -- yaliiweka PSG katika udhibiti thabiti kabla ya Khvicha Kvaratskhelia and mtoka benchi Senny Mayulu kupigilia misumari ya mwisho kwenye jeneza lilloizika Madrid.

Mashabiki wa PSG na mabango ya uungaji mkono wao kwa Palestina

 

Jijini Paris, furaha isiyo na kifani ilitawala wakati mashabiki walimiminia barabarani, wakipunga skafu za PSG kutoka kwenye madirisha ya magari na kuwasha fataki kusherehekea ushindi huo wa kwanza wa timu hiyo wa Ligi ya Mabingwa. Lakini sherehe hizo ziligeuka kuwa za machafuko katika Ikulu ya Champs-Elysees, ambapo polisi walifyatua mabomu ya gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha ili kutuliza ghasia hizo. Inaarifiwa kuwa, watu 2 wameuawa huku wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa kwenye vurumai hizo.

Hata hivyo tukio lililovutia zaidi wakati wa mechi hiyo, ni pale mashabiki wa PSG walipotangaza himaya na uungaji mkono wao kwa Palestina. Katika mechi hiyo ya fainali iliyochezwa katika Uwanja wa Allianz Arena mjini Munich, Ujerumani, mashabiki wa timu hiyo walikuwa na bendera kubwa ya Palestina na maberamu yaliyokuwa na maandishi ya kuunga mkono Palestina. Mashabiki wa Paris Saint-Germain wakiwa katika Uwanja wa Allianz Arena mjini Munich, walilaani vikali vitendo vya kikatili vya utawala ghasibu wa Kizayuni na kushikilia bendera ya kuiunga mkono Palestina. Beramu kubwa lililokuwa limebebwa na mashabiki wa PSG lilisomeka: "Komesheni mauaji ya kimbari huko Gaza."

Na inaelekea kuwa, ndoa ya kisoka kati ya mwanakandanda nyota, Cristiano Ronaldo na klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia inaelekea kuvunjuka. Ronaldo, muda mfupi baada ya mechi ya mwisho ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Saudia Jumatatu ya wiki iliyopita, alirusha ujumbe usio wa moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii, akiashiria kwamba alikuwa amecheza mechi yake ya mwisho kwenye klabu hiyo. Mkataba wa sasa wa Ronaldo na Al Nassr unamalizika mwezi huu wa Juni.

Cristiano Ronaldo anaondoka klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia?

Haielekei kuwa Ronaldo atastaafu, ingawaje, akiwa na umri wa miaka 40, wachambuzi wa spoti wanasema angeliweza kuangika daluga, na kuamua kuondoka kama mmoja wa wachezaji bora zaidi wa soka duniani.

………………….MWISHO…..………..