Ulimwengu wa Spoti, Mei 26
Ahlan wasahlan mpenzi mwanaspoti. Kwa moyo mkunjufu nakukaribisha tuangazie baadhi ya matukio muhimu yayojiri viwanjani ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa…..
Timu ya Iran ya Para-Karate bingwa wa Asia 2025
Timu ya taifa ya Iran ya Para-Karate imenyakua taji la ubingwa katika Mashindano ya Asia ya 2025 yaliyofanyika Tashkent, Uzbekistan. Makarateka hao wa Iran wenye ulemavu wa akili wametwaa ubingwa baada ya kumaliza kwa jumla ya medali 2 za dhahabu, 3 za fedha na 2 za shaba. Ushindi huu hauangazii tu kuongezeka kwa uwezo wa para-karate nchini Iran bali pia ni mafanikio makubwa katika kukuza ushirikishwaji na uwakilishi katika michezo kwa wanariadha wenye ulemavu. Timu ya Iran ilitawala mashindano hayo, ikifanya vyema zaidi huku Kazakhstan iliyoshika nafasi ya pili ikipata medali 2 za dhahabu, 1 ya fedha na 4 za shaba, huku Saudi Arabia ikimaliza ya tatu kwa medali 1 ya dhahabu, 2 za fedha na 4 za shaba.

Michuano hii inaashiria mwendelezo wa mafanikio ya Iran katika para-karate, kwani pia walitwaa taji hilo katika toleo la awali la mashindano hayo. Washindi wa medali kutoka Iran walionyesha vipaji vya hali ya juu na umahiri mkuubwa katika mashindano hayo. Walionyakua medali za dhahabu katika mashindano hayo kwa upande wa Iran ni Masoumeh Iji, ambaye alishinda dhahabu katika kitengo cha K21 kwa wanariadha wenye ulemavu wa akili na Farzad Safari, ambaye pia alipata dhahabu katika kitengo cha K22 kwa wanariadha wenye ugonjwa wa Down.
Karate: Wairani watwaa medali Uzbekistan
Sara Bahmanyar wa Iran alishinda medali ya shaba katika Mashindano ya Mabingwa ya AKF ya 2025 yanayofanyika Tashkent, Uzbekistan. Alimchakaza Ibaa Salama ya Palestina kwa alama 5-3 katika pambano lake la ufunguzi lakini akashindwa na Gulshan Alimardanova wa Uzbekistan kwa 2-1. Bahmanyar kisha alipata ushindi mara mbili dhidi ya Arnella Putri Wandari wa Indonesia kwa pointi 7-0 na Mchina Taipei Hsin-Yu Chan kwa 4-3. Wakati huo huo, timu ya wanaume ya Iran ya Karate mtindo wa Kata imetwaa medali ya shaba katika mashindano hayo siku ya Jumamosi. Timu hiyo ya Iran iliishinda Vietnam katika mechi ya kutafuta mshindi wa pili na kutwaa medali ya shaba. Mashindano hayo yamefanyika Tashkent kuanzia Mei 23 hadi 25. Mashindano hayo yanatumika kama kufuzu kwa Mashindano ya Dunia ya Mtu Mkubwa ya 2025, yaliyopangwa kufanyika Novemba huko Cairo, Misri.
Mieleka Asia; Wanawake wa Iran wang'ara
Timu ya wanamieleka ya wanawake ya Iran ya Alish imetwaa taji la ubingwa katika Mashindano ya Mieleka ya Asia, baada ya kujinyakulia medali tatu za dhahabu, medali mbili za fedha na medali moja ya shaba katika kitengo cha classic. Timu ya Iran ilipata mafanikio makubwa ambapo Roghayeh Mahmoudabadi alishinda dhahabu katika kitengo cha kilo 65, Mobina Mirzapur katika kitengo cha kilo 70, na Sahar Ghanizadeh katika kitengo cha kilo 75. Marzieh Khandan alipata medali ya fedha katika kitengo cha kilo 55, Fatemeh Fattahi katika kitengo cha kilo 60, na Ezzat Ghorbani Sani alipata shaba katika kitengo cha kilo +75. Iran iliongoza orodha ya timu kwa pointi 130, ikifuatiwa na Kazakhstan pointi 110, Kyrgyzstan pointi 105, na India pointi 75. Mashindano ya mieleka ya Alish katika kitengo cha mitindo huru yamepangwa kufanyika leo, ambapo wawakilishi wa Iran watachuana na wapinzani wao. Michuano hiyo ilifanyika New Delhi, India, ambapo timu ya Iran ilifanikiwa kutetea ubingwa wake dhidi ya washindani wenye nguvu. Utendaji huo unaonyesha kina cha talanta ndani ya mpango wa mieleka wa wanawake wa Irani na kujitolea kwake kwa ubora.
Kombe la Hazfi
Timu ya kandanda ya Malavan iliitandika Gol Gohar bao 1-0 siku ya Ijumaa na kujihakikishia nafasi ya kucheza fainali ya Kombe la Mtoano la Iran (Kombe la Hazfi) 2024/25. Reza Jafari ndiye aliyefunga bao hilo la pekee na na la ushindi katika dakika ya 76 ya mchezo. Nusra goli hilo likataliwe ikidhaniwa ni la kuotea, lakini VAR ikaamua si la kuotea.

Jumamosi usiku, Esteghlal walikuwa wenyeji wa Sanat Naft katika Uwanja wa Azadi wa Tehran katika nusu fainali nyingine. Na kama ilivyotarajiwa, The Blues wa Tehran waliutandaza mpira wa kuwanyuka wageni mabao 2-0, Mkenya Masoud Juma akicheka na nyavu katika goli la pili. Esteghlal hiyo itachuana sasa na Malavan katika kitimitimu cha fainali Alkhamisi ijayo ya Mei 29. Nikudokeze tu kwamba, Esteqlal inasalia klabu yenye mafanikio zaidi katika historia ya Kombe la Hazfi, ikiwa imeshinda taji hilo mara saba. Malavan wametwaa kombe hilo mara tatu. Kombe la Hazfi ni shindano la kila mwaka la mtoano la soka linaloandaliwa na Shirikisho la Soka la Iran. Mechi ya mwisho imeratibiwa kufanyika katika Uwanja wa Arak's Imam Khomeini mnamo Mei 29.
Simba mla nyasi alazwa chali
Kwenye habari ya tuseme ya tanzia, maana ndo wameibuka na msemo sasa eti simba mla nyasi kalazwa chali. Mambo yaliiendelea segemnege klabu ya Simba ya Tanzania iliposhuka dimbani kucheza mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco ambayo ilipigwa Jumapili.

RS Berkane ya Morrocco imetwaa ubingwa wa michuano hiyo ya kikanda kwa mara ya tatu katika historia, kufuatia ushindi wa jumla wa mabao 3-1 dhidi ya Simba katika dimba la New Amaan Complex, visiwani Zanzibar. Simba ililazimishwa sare ya bao 1-1 Jumapili, na hivyo kupoteza fainali nyingine, tena mbele ya Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi kama ilivyokuwa mwaka 1993 ilipopoteza fainali nyingine mbele ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi, baba yake ya Dkt. Mwinyi. Ndiyo historia hiyo na tabia yake ya kupenda kujikariri. Simba walianza mchezo kwa kasi nzuri, wakionesha mbinu na kiu ya ushindi. Wachezaji walikuwa na muunganiko mzuri na walimiliki sehemu kubwa ya mchezo kwa muda. Lakini hali hiyo haikudumu baada ya mchezaji mmoja kutolewa kwa kadi nyekundu – tukio ambalo lilibadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo huo wa fainali. Moja kati ya matukio yaliyotikisa mchezo huo ni tukio la Fabrice Ngoma na Moussa Camara, nyota wa klabu ya Simba kupigana muda mfupi baada ya kutamatika kwa kipindi cha kwanza cha mchezo huo, baada ya kutofautiana. Tunawapa pole ndugu zetu, Wekundu wa Msimbazi. Asiyekubali kushindwa si mshindani, tujaribu msimu ujao labda.
Pyramid na Mamelodi ngoma droo
Klabu ya soka ya Pyramids ya Misri ilifanikiwa kusawazisha katika dakika za lala salama na kuambulia sare ya bao 1-1 na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, katika mechi ya mkondo wa kwanza wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi. Huku sheria ya bao la ugenini ikiwa bado inatumika katika mashindano ya klabu barani Afrika, kasi sasa inazidi kuimarika kwa klabu hiyo ya Cairo baada ya Walid El Karti kupachika wavuni kwa kichwa baada ya kumaliza kwa nguvu, katika mchezo uliochezwa katika uwanja wa Loftus Versfeld. Sundowns walikuwa wamepata bao la kuongoza kupitia kwa kiungo Mbrazil, Lucas Ribeiro katika dakika ya 54 kwa shuti kali la mguu wa kushoto baada ya pasi kumpata vyema. Mechi ya marudiano baina ya timu mbili hizo itasakatwa katika Uwanja wa Ulinzi wa Ndege wa Cairo Jumapili ijayo, Juni 1. Pyramids FC haijawahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na Mamelodi Sundowns imechukua ubingwa huo mara moja 2016.
Dondoo za Hapa na Pale
Tottenham iliifunga Manchester United bao 1-0 na kushinda fainali ya Ligi ya Europa, na kunyanyua taji lake la kwanza la bara Ulaya baada ya zaidi ya miongo minne, na sasa wamefuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Hilo ni taji la kwanza kuu kwa Tottenham tangu ilipotwaa Kombe la Ligi ya Uingereza mwaka 2008, na ushindi wake wa kwanza wa Uropa tangu iliposhinda Kombe la UEFA kwa mara ya pili - sawa na Ligi ya Europa sasa - mnamo 1984. Brennan Johnson alifunga bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha kwanza katika mchuano huo wa aina yake siku ya Jumatano na kuisaidia Spurs kuokoa msimu mbaya, ambapo itamaliza ikiwa mkiani kabisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza EPL. Ushindi huo unakuja miaka sita baada ya Tottenham kukosa ushindi dhidi ya Liverpool kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa. Man U hiyo, siku ya Jumapili walimaliza msimu wao wa kusikitisha wa 2024-25, kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Aston Villa katika siku ya mwisho ya kampeni ya Ligi ya Premia, na kuwanyima wageni nafasi ya kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa.

Wakati huo huo, msimu wa kutatanisha wa Manchester City ulimalizika kwa kufarijiwa kwa kupata tiketi ya Ligi ya Mabingwa, baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Fulham, uliopatikana kwa mkwaju wa juu wa kichwa wa Ilkay Gundogan na mkwaju wa penalti wa Erling Haaland.
Mabingwa Liverpool walimaliza kampeni zao kwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Crystal Palace kwenye uwanja wa Anfield ambapo baadaye walipokezwa kombe lao la EPL kwa kumaliza kidedea kwa alama 84. Washindi wa pili Arsenal, ambao walimaliza kwa pointi 10 nyuma ya Liverpool, waliifunga klabu inayovuta mkiani Southampton mabao 2-1 wakiwa ugenini.
Mbali na hayo, klabu ya Napoli imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Italia (Serie A) baada ya kuinyuka Cagliari mabao 2-0, mabao ya timu hiyo yakifumwa wavuni na Scott McTominay na Romelu Lukaku.
Na watu watano wamehukumiwa kifungo jela kwa kumdhalilisha mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Jr wakati wa mechi, katika uamuzi wa kwanza wa kihistoria nchini Uhispania dhidi ya matusi ya kibaguzi uwanjani kama uhalifu wa chuki, hayo ni kwa mujibu wa La Liga. Mnamo Desemba 30, 2022, nguli huyo wa kimataifa wa Brazil, alidhulumiwa katika ushindi wa mabao 2-0 wa Real ugenini kwenye uwanja wa Jose Zorrilla dhidi ya Real Valladolid alipokuwa akiwapita mashabiki baada ya kubadilishwa. Mahakama ya Mkoa wa Valladolid Jumatano iliwahukumu wahalifu hao watano kifungo cha mwaka gerezani na faini ya kuanzia euro 1,080 ($1,226.12) hadi euro 1,620 ($1,836). Vifungo hivyo vimesitishwa kwa sharti la kutotenda kosa lolote katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, na pia hawataruhusiwi kuhudhuria mechi yoyote katika kipindi hicho. Safi sana, kidogo inatia matumaini.
………………..MWISHO……………