Rais wa Ufaransa azabwa kibao na mkewe hadharani + Video
Kitendo cha mke wa Rais wa Ufaransa cha kumzaba kibao mumewe hadharani mara baada ya kuwasili kwa ndege nchini Vietnam, kimempiga bumbuwazi Rais Emmanuel Macron aliyezabwa kibao hicho na kila aliyeangalia video hiyo.
Video inayoonesha mke wa Macron akimzaba kibao mumewe na baadaye kukataa kumshika mkono wakati wanashuka ndege, imeenea kwa kasi ya umeme mitandaoni. Video hiyo iliyoenea sana kwenye mitandao ya kijamii inamuonesha mke wa rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Bi Brigitte Marie-Claude Macron ambaye ni bikizee wa miaka 72, akimpiga kibao cha uso mumewe baada ya ndege yao kutua Vietnam.
Macron aliwasili Vietnam jana Jumapili kama sehemu ya safari yake ya kuzitembelea nchi za Asia. Macron alionekana kushtushwa na kitendo cha mkewe lakini akajaribu kujizuia mbele ya kamera.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amepigwa kibao na mkewe Brigitte alipowasili Vietnam, na kwamba Brigitte alikataa kumshika mkono mumewe walipokuwa wakishuka kwenye ndege. Ikulu ya Ufaransa Elysee imefanya juhudi za kufifiliza tukio hilo bila ya mafanikio.
Kwa upande mwingine, rafiki mmoja wa rais wa Ufaransa amesema kuwa Macron na mkewe walikuwa na "mabishano madogo" walipofika Hanoi.
Ikulu ya Ufaransa imethibitisha usahihi wa video hiyo na kusema ni kweli tukio hilo limetokea.
Kabla ya hapo redio ya Ufaransa RMC BFM iliripoti kwamba Paris awali ilisema kuwa, huenda video hiyo imetengenezwa kwa Akili Mnemba na kutumwa mtandaoni na akaunti zinazoiunga mkono Russia, lakini baadaye Ikulu ya Ufaransa imethibitisha usahihi wa video hiyo.