Almasi Zilizochongwa kwa Machozi ya Afrika-Sehemu ya Kwanza: Maumivu ya Ukoloni
https://parstoday.ir/sw/news/event-i138748-almasi_zilizochongwa_kwa_machozi_ya_afrika_sehemu_ya_kwanza_maumivu_ya_ukoloni
Wapenzi wasikilizaji, Ukoloni wa karne ya kumi na tisa haukuwa wa kuhodhi ardhi tu za mataifa, bali ulikuwa mfumo na utaratibu maalumu ulioratibiwa kwa ajili ya kuuhamisha utajiri wa Afrika na kuupeleka Ulaya. Katika kipindi kilichojulikana kama “ Uvamizi wa Afrika”, Uingereza ilitumia nguvu zake za kiuchumi pamoja na makampuni binafsi kuanzisha ubeberu wa kimuundo na ulio endelevu wa kuzihodhi rasilimali za bara hilo.
(last modified 2026-05-30T08:46:00+00:00 )
May 30, 2026 08:17 UTC
  • Maumivu ya Ukoloni na Almasi Zilizochongwa kwa Machozi ya Afrika
    Maumivu ya Ukoloni na Almasi Zilizochongwa kwa Machozi ya Afrika

Wapenzi wasikilizaji, Ukoloni wa karne ya kumi na tisa haukuwa wa kuhodhi ardhi tu za mataifa, bali ulikuwa mfumo na utaratibu maalumu ulioratibiwa kwa ajili ya kuuhamisha utajiri wa Afrika na kuupeleka Ulaya. Katika kipindi kilichojulikana kama “ Uvamizi wa Afrika”, Uingereza ilitumia nguvu zake za kiuchumi pamoja na makampuni binafsi kuanzisha ubeberu wa kimuundo na ulio endelevu wa kuzihodhi rasilimali za bara hilo.

Katika kipindi kilichojulikana kama “ Uvamizi wa Afrika”, Uingereza ilitumia nguvu zake za kiuchumi pamoja na makampuni binafsi kuanzisha ubeberu wa kimuundo na ulio endelevu wa kuzihodhi rasilimali za bara hilo.Ukoloni katika karne ya kumi na tisa, haukuwa wa uvamizi wa kijeshi pekee. Ulikuwa ni mtandao wa nguvu za kisiasa, mitaji ya kifedha na sheria za kibaguzi zilizowekwa ili kutumia rasilimali za nchi za mbali kwa manufaa ya maendeleo ya kiviwanda ya Ulaya. Wakati wa kile kilichoitwa “Uvamizi wa Afrika”, bara hilo liligawanywa kati ya mataifa ya Ulaya, huku Dola kuu la Uingereza likiwa mmoja wa wahusika wakuu wa mpango huo; ambapo kupitia makampuni binafsi na kwa kutumia mbinu za kiuchumi, Waingereza waliweza kuzatiti satua yao na kuendeleza mfumo wa kunyonya utajiri wa Afrika kwa muda mrefu.Ugunduzi wa almasi nchini Afrika Kusini katika miaka ya 1860 yalikuwa mabadiliko muhimu ya mchakato huo. Kugunduliwa kipande cha almasi kando ya Mto Orange katika mwaka 1867 kuliibua joto kubwa la uchu na tamaa ya kujipatia utajiri; na mji wa Kimberley ukageuka kuwa kitovu cha uchimbaji wa almasi. Shimo kubwa lililojulikana kama “Big Hole” likawa alama na nembo ya zama hizo; zama zilizobadilisha kikamilifu mfumo wa kijamii wa eneo hilo.Kadiri thamani ya migodi ilivyoongezeka, ndivyo serikali ya kikoloni ilivyoingilia suala la umiliki wa ardhi na sheria za madini. Maelfu ya watu waliokuwa wakisaka utajiri walimiminika katika eneo hilo, ardhi za wenyeji zikawekewa vizuizi na kuporwa, na kupelekea kudhoofika mifumo ya jadi ya kijamii.Mwaka 1888, na baada ya kuunganishwa kampuni ndogo ndogo, kampuni ya De Beers iliasisiwa, ambayo ilidhibiti sehemu kubwa ya uchimbaji wa almasi duniani. Mwenendo huo uliongozwa na Cecil Rhodes, bepari na mwanasiasa ambaye baadaye alikuja kuwa Waziri Mkuu wa koloni la Cape. Rhodes alitumia mapato ya migodi kupanua ushawishi wa Uingereza kuelekea kaskazini mwa Afrika. Ardhi zilizokuja baadaye kupewa jina la Rhodesia zilitokana na jina lake, ikiwa ni ishara ya wazi ya mfungamano uliokuwepo kati ya mtaji wa madini na upanuzi wa ardhi zilizokuwa chini ya mamlaka ya ukoloni.Katika kipindi hicho, almasi haikuwa tena jiwe la thamani tu, bali iligeuzwa kuwa wenzo wa kijiopolitiki. Utajiri wa Kimberley ulikuwa nguzo muhimu ya kuimarisha ushawishi wa Uingereza kusini mwa Afrika, ambapo uchimbaji wa almasi ulitumika kuhalalisha na kuendeleza ubeberu wa kisiasa na kiuchumi wa Dola kuu la kikoloni.Hata hivyo, wenyeji wa eneo hilo ndio walilobeba mzigo wa kugharimia kupanuka kwa satua hiyo ya ubeberu. Katika miongo ya mwisho wa karne ya kumi na tisa, sekta ya madini iliweka mifumo ambayo, baadaye ilikuja kuwa msingi wa utawala wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid — mfumo uliolenga kudhibiti nguvukazi, kuhalalisha utovu wa usawa, na kuimarisha ulimbikizaji wa utajiri mikononi mwa wachache.Miongoni mwa hatua za mwanzo zilizochukuliwa na wamiliki wa migodi ili kuzuia wizi wa almasi ilikuwa ni kuanzisha makazi maalumu yaliyowekewa uzio, maarufu kama compound. Ndani ya eneo hilo lililofungiwa, wafanyakazi weusi wa vibarua, wengi wao wakitoka vijijini na maeneo ya kikabila walivutwa na matumaini ya kupata mshahara wa fedha taslimu. Lakini walipowasili migodini waliwekwa katika maeneo yaliyokuwa yamezungushiwa uzio mkali. Maeneo hayo yalidhibitiwa kwa uzio mrefu na walinzi wenye silaha, na wafanyakazi hawakuruhusiwa kutoka kwa uhuru mpaka mikataba yao ya kazi ilipomalizika.Ukaguzi wa mara kwa mara wa kupekuliwa miili, usajili makini wa kuingia na kutoka, pamoja na udhibiti wa afya na chakula, vyote vilikuwa sehemu ya mfumo huo uliowekewa nidhamu kali. Kile kilichokuwa kikielezwa kama hatua kali za kiusalama, kiuhalisia ilikuwa aina ya kifungo cha viwandani kilichobana kwa kiwango kikubwa maisha binafsi na uhuru wa vibarua.

Mfumo huo haukuishia tu katika maeneo ya makazi ya wafanyakazi. Hata mfumo wa kazi migodini ulijengwa juu ya msingi wa ubaguzi wa rangi. Kazi za kitaalamu, usimamizi na nafasi za juu walitengewa wafanyakazi wazungu, huku wafanyakazi weusi wakipewa kazi ngumu za mikono na zilizokuwa hatarishi mno. Mishahara ilifanywa kimpangilio iwe tofauti na hakukuwa na uwezekano wa wafanyakazi weusi kupandishwa vyeo. Kwa utaratibu huo, sekta ya migodi ikawa eneo la kwanza, ambapo mgawanyo wa kazi ulifanywa kimpangilio kwa misingi ya rangi za watu na ambao hatimaye ulienea katika sekta nyingine za kiuchumi.Hatua kwa hatua, mfumo huo wa ubaguzi na wa utovu wa usawa uliingizwa kwenye sheria rasmi za ajira, na baadaye ukawa moja ya nguzo kuu za mfumo wa kibaguzi wa Afrika Kusini — mfumo ambao katika miaka iliyofuatia ulijulikana rasmi kama Apartheid.Sheria za “Paspoti” au “Pass Laws” zilidhibiti harakati na ingia toka za Waafrika weusi. Mtu aliyekutwa hana kitambulisho maalumu cha ukazi aliishia korokoroni. Mfumo huo wa kiutawala baadaye ulihalalishwa rasmi chini ya sera ya Apartheid.Kwa ajili ya kuhakikisha inapata wafanyakazi wa gharama nafuu, serikali ya kikoloni iliweka kodi za kichwa na wakati huo huo ikapunguza umiliki wa ardhi kwa wenyeji. Vijana wengi wa Kiafrika walilazimika kwenda kufanya kazi migodini ili kulipa kodi na kuendesha maisha yao. Hapo ndipo ulipozaliwa mfumo wa “migrant labour” au mfanyakazi mhamiaji; mfumo ambao ulizitenganisha familia na kusababisha utegemezi wa kiuchumi.Ilikuwa ni katika kipindi hicho hicho, ambapo ulimbikizaji wa mitaji mikononi mwa Wazungu wachache ulishika kasi. Kwa kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa almasi duniani, kampuni ya De Beers iliunda kampuni yenye nguvu kubwa iliyoweza hata kupanga bei ya almasi katika soko la dunia. Faida kubwa ilipelekwa London, wakati gharama za maafa ya kibinadamu zilibaki Afrika Kusini. Huu ndio uliokuwa mfumo wa uchumi wa kikoloni wa uchimbaji: rasilimali zilichukuliwa pembezoni mwa dunia, lakini thamani yake ilikusanywa katika mataifa ya kikoloni.Ushirikiano kati ya serikali ya kikoloni na makampuni ya migodi uliimarisha mzunguko huo. Sheria za kuzuia umiliki wa ardhi kwa Waafrika pamoja na sera za ubaguzi wa kazi zilihakikisha kuwa sekta ya madini inaendelea kuingiza faida kubwa kwa watawala wa kikoloni. Na ilipofika mwaka 1948, wakati Apartheid ilipotangazwa rasmi nchini Afrika Kusini, mifumo mingi ya utawala huo ilikuwa tayari imeshajaribiwa ndani ya sekta ya migodi. Sekta ya almasi haikuzalisha utajiri pekee, bali pia ilitengeneza mfumo kamili wa udhibiti wa watu kwa misingi ya rangi zao.Katika karne ya ishirini, kampuni ya De Beers ilihodhi karibu biashara yote ya almasi ghafi duniani. Kupitia kampeni yake maarufu ya mwaka 1947 yenye kauli mbiu “A Diamond is Forever” (yaani Almasi ni ya Milele), kampuni hiyo ilikigeuza kito hicho kuwa alama ya mapenzi na ndoa katika jamii za Magharibi.Lakini wakati almasi inatangazwa kama nembo ya mahaba huko Ulaya na Marekani, wafanyakazi Waafrika waliendelea kufanya kazi migodini katika mazingira magumu na hatarishi. Faida zilikuwa zikimiminika katika vituo vya kifedha vya Magharibi, huku jamii za wenyeji huko Afrika zikiatilika kwa ufukara na kubaki bila ya ardhi. Huo ndio uliokuwa msingi wa uchumi wa kikoloni: mateso pembezoni mwa dunia, starehe katikati ya waliokuwa na himaya.Ikiwa leo hii mtu ataitazama hali ya mgawanyo wa ardhi na utajiri isiyo na usawa nchini Afrika Kusini, ataona wazi alama za mfumo ule ule uliojengwa katika karne ya kumi na tisa chini ya kivuli cha bendera ya dola kuu la Uingereza. Uchimbaji wa almasi haukuzaa utajiri tu, bali ulijenga pia mfumo wa ubeberu na utovu wa usawa uliodumu kwa vizazi vingi. Mng’aro wa almasi za Kimberley ni kioo cha historia yenye giza iliyozaliwa kwenye kitovu cha ukoloni na mateso ya raia wenyeji wa Afrika. Kile ambacho leo hii kinajulikana kama almasi kikionekana kinang’ara kwenye maonesho ya vito duniani si jiwe la thamani tu; ni sehemu ya historia ya utovu wa usawa ambao hadi leo ungali unatweta ndani ya mishipa ya mfumo wa umiliki wa ardhi na mgawanyo wa utajiri nchini Afrika Kusini.

Huenda suali halisi la kuulizwa lisiwe ni almasi ina thamani gani, bali ni kina nani waliolipia gharama yake, na ambao hadi hii leo wanaendelea kufanya hivyo.

Kwa nini “Somaliland” imeipendekezea Marekani kuanzisha kambi ya kijeshi katika eneo hilo?

Somaliland imetoa pendekezo kwa Marekani la kuanzisha kambi ya kijeshi katika eneo hilo.Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, viongozi wa Somaliland wameipendekezea Washington kutumia rasilimali za madini zilizopo katika eneo hilo pamoja na kuanzisha kituo cha kijeshi.Khadr Hussein Abdi, Waziri wa Masuala ya Urais wa eneo linalojulikana kama Somaliland, amesema:“Tuko tayari kuipatia Marekani haki ya kutumia migodi yetu pamoja na kuanzisha vituo vya kijeshi.”Ameongeza kuwa, pendekezo hilo lina lengo la kuisaidia Somaliland kupata uhalali na kukubalika kimataifa.Khadr Hussein Abdi amebainisha pia kuwa, viongozi wa eneo hilo wako tayari kuipatia Marekani haki ya kipekee ya kutumia rasilimali za madini pamoja na kuanzisha vituo vya kijeshi.Pendekezo hilo linatolewa wakati ambapo utawala wa Kizayuni wa Israel mnamo Desemba 2025 uliitambua Somaliland kama nchi huru, suala lililokabiliwa na mijibizo mikali na malalamiko makubwa kikanda na kimataifa. Nchi kama Misri, Jordan, Djibouti, Saudi Arabia na Uturuki zilionyesha upinzani wao dhidi ya hatua hiyo. Aidha, nchi 20 kutoka Asia Magharibi na Afrika zilitoa tamko la pamoja kulaani hatua hiyo ya utawala wa kizayuni .Wakati huo huo, hatua zinazochukuliwa na serikali ya shirikisho ya Somalia kuzuia kuthibiti mipango na njama hatari za Israel katika eneo la Somaliland hazionekani kuwa jibu tu kwa harakati za eneo hilo linalotaka kujitenga na nchi hiyo, lakini pia kama sehemu ya mkakati mpana wa kulinda umoja wa kitaifa, kuzuia uingiliaji wa kigeni na kuimarisha mamlaka ya serikali kuu katika moja ya maeneo hasasi na muhimu zaidi barani Afrika.Kwa sasa inavyoonekana, eneo linalojiendeshea masuala yake ya ndani la Somaliland limeanzisha juhudi mpya za kutafuta uungaji mkono na kutambuliwa rasmi kimataifa kwa kuipatia Marekani pendekezo la kuanzisha kambi ya kijeshi pamoja na haki ya kipekee ya kutumia rasilimali zake za madini. Hatua hii inachukuliwa ikikumbukwa kuwa, Somaliland ilijitangazia uhuru tangu mwaka 1991, lakini hadi leo bado haijatambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa wala serikali ya shirikisho ya Somalia, ambayo ingali inaichukulia Somaliland kama sehemu ya ardhi ya nchi hiyo.Sababu kuu za kutolewa pendekezo hilo kwa Marekani zinaweza kuchunguzwa katika nukta kadhaa muhimu. Ya kwanza na yenye uzito mkubwa zaidi ni juhudi za Somaliland za kutaka kujinasua kwenye kinamasi cha hali ya kutengwa kidiplomasia. Licha ya kuwa na serikali, jeshi na sarafu yake kwa muda wa miongo mitatu sasa, Somaliland haijaweza kutambuliwa rasmi kimataifa.Kwa hiyo pendekezo ililotoa kwa Marekani linaonekana kama mwendelezo wa harakati iliyoanza Desemba 2025 baada ya eneo hilo kutambuliwa na Israel. Viongozi wa Somaliland wana tamaa kwamba kwa kujigeuza kuwa mshirika wa kimkakati wa Washington, neo hilo litaweza pia kuvutia uungaji mkono wa mataifa mengine makubwa duniani.Nukta ya pili ni nafasi hasasi na muhimu sana ya kijiopolitiki ya Somaliland. Eneo hilo lipo kwenye mwambao wa Ghuba ya Aden, likiwa mkabala moja kwa moja na Yemen. Kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na harakati ya Muqawama ya Yemen dhidi ya meli zenye uhusiano na utawala wa Kizayuni zinazopita katika njia hiyo muhimu ya baharini, uwepo wa kituo cha kijeshi katika pwani ya kusini ya Ghuba ya Aden unaonekana kuwa na umuhimu mkubwa kijeshi na kiusalama kwa Marekani na washirika wake.Eneo hilo linaweza kutumiwa kama kituo cha ufuatiliaji na utoaji mijibizo ya haraka kwa matukio yanayojiri Yemen pamoja na kulinda usalama wa njia za meli, tab’an kwa maslahi ya Magharibi na Tel Aviv.Nukta na sababu ya tatu muhimu ni utajiri wa rasilimali za madini uliotajwa kuwepo katika eneo hilo. Viongozi wa Somaliland wanasema, kuna akiba kubwa ya madini muhimu sana kama lithium na coltan, yanayohitajika mno duniani katika viwanda vya teknolojia ya kisasa na sekta ya ulinzi. Japokuwa bado hazijafanyika tafiti huru za kuthibitisha kiwango halisi cha akiba iliyopo ya rasilimali hizo, lakini huo uwezekano tu unatumiwa kama wenzo madhubuti wa kuivutia Marekani.Pendekezo hili linaweza kuwa na matokeo kadhaa. Kwa upande mmoja, makubaliano yoyote ya kijeshi yatakayofikiwa kati ya Marekani na Somaliland yanaweza kuharibu zaidi uhusiano wa Washington na serikali ya shirikisho ya Somalia. Viongozi wa Somalia wameashiria mkataba uliosainiwa kitambo nyuma tangu mwaka 1980 kati ya nchi hiyo na Marekani wakisisitiza kwamba, ushirikiano wa kijeshi baina ya pande mbili inapasa ufanyike kwa mujibu wa kisheria na kupitia serikali kuu, na kwamba makubaliano mengine yoyote ya kando yanakinzana na mamlaka ya kujitawala ya Somalia.Kwa upande mwingine, hatua hiyo ya Somaliland inaweza kushadidisha mivutano katika eneo la Pembe ya Afrika.Na mwisho ni kuwa, hata kama hadi sasa serikali ya Marekani haijatoa msimamo rasmi kuhusu suala hilo, sambamba na Donald Trump kufuta uwezekano wa kuitambua rasmi Somaliland, lakini pendekezo hilo linadhihirisha wazi mabadiliko yanayojiri katika mizani ya milingano ya nguvu na ushindani ya kujijengea satua na ushawishi katika Pembe ya Afrika…/