Rais Raisi: Uingiliaji wa maajinabi unayafanya mambo yazidi kuwa tata tu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100286-rais_raisi_uingiliaji_wa_maajinabi_unayafanya_mambo_yazidi_kuwa_tata_tu
Rais Ebrahim Raisi amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono mazungumzo ya kuleta amani kati ya Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan na kusisitiza kuwa, uingiliaji wa wageni unayafanya mambo yawe tata tu zaidi.
(last modified 2026-07-28T12:43:49+00:00 )
Jul 25, 2023 00:47 UTC
  • Rais Raisi: Uingiliaji wa maajinabi unayafanya mambo yazidi kuwa tata tu

Rais Ebrahim Raisi amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono mazungumzo ya kuleta amani kati ya Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan na kusisitiza kuwa, uingiliaji wa wageni unayafanya mambo yawe tata tu zaidi.

Rais Raisi ameyasema hayo katika mazungumzo na Ararat Mirzoyan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Armenia aliyewasili Tehran jana kwa lengo la kukutana na kushauriana na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
 
Katika mazungumzo hayo, Seyed Ebrahim Raisi amesema: "Uingiliaji wa maajinabi unayafanya mambo yawe magumu tu zaidi, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuunga mkono mazungumzo ya amani kati ya Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan, inatumai kuwa mazungumzo hayo yatawezesha kupatikana na kuimarishwa zaidi amani, usalama na utulivu katika eneo ".
 
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Rais Raisi aidha ameeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikubaliani na kufanywa mabadiliko yoyote ya kijiografia na kubadilisha mipaka ya nchi za eneo na kuongeza kuwa: Iran inaunga mkono mamlaka na umoja wa ardhi wa nchi zote za eneo.
Ararat Mirzoyan (kushoto) alipokutana na mwenzake wa Iran Hossein Amir-Abdollahian

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuboreshwa zaidi kiwango cha uhusiano kati ya nchi hizo mbili kadiri na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haioni kama kuna kikwazo chochote cha kupanuliwa uhusiano kati yake na Armenia.

 
Katika mazungumzo hayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Armenia ameshukuru na kupongeza misimamo ya Iran kuhusiana na matukio ya eneo la Caucasus na kusema: Armenia katu haitakuwa uwanja wa kuchukulia hatua dhidi ya Iran na daima inasisitiza juu ya kustawishwa usalama na amani ya eneo.
 
Aidha Mirzoyan amesema, uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran una umuhimu mkubwa sana kwa nchi yake na akasisitiza juu ya kuongezwa kiwango cha mawasiliano ya kidiplomasia kati ya nchi mbili na kuimarishwa zaidi uhusiano baina yao.../