Jul 26, 2023 03:10 UTC
  • Iran: Mkono wa Israel unaonekana kwenye vitendo vya kuivunjia heshima Qur'ani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya Magharibi za Sweden na Denmark na kusema kuwa, alama za vidole za utawala haramu wa Israel zinaonekana wazi kwenye vitendo hivyo viovu.

Nasser Kan'ani alisema hayo jana Jumanne kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, "Mkono wa nyuma ya pazia wa utawala wa Kizayuni unaoneka dhahiri kwenye (vitendo vya) hujuma dhidi ya Qurani Tukufu."

Amezikosoa vikali nchi za Magharibi zinazodai kuwa kukivunjia heshima Kitabu Kitakatifu cha Waislamu zaidi ya bilioni mbili duniani kwao ni uhuru wa kujieleza, akisisitiza kuwa misimamo hiyo inadhihirisha undumakuwili wa Wamagharibi.

Kan'ani amesema pamoja na kuhusika Israel kwenye vitendo hivyo vya kuivunjia heshima Qurani Tukufu, lakini serikali za Sweden na Denmark zinapaswa kubebeshwa dhima kwa kutoa idhini ya kufanyika uafriti huo dhidi ya matukufu ya Kiislamu.

Baada ya raia mmoja wa Sweden kuivunjia heshima tena Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Stockholm Alkhamisi iliyopita, genge jingine lenye misimamo mikali ya kulia lilimuunga mkono mtenda jinai huyo kwa kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Copenhagen, Denmark.

Nembo ya OIC

Kadhalika Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameipongeza na kuishukuru Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa kukubali mwito wa kufanyika kikao cha dharura cha taasisi hiyo kujadili kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani nchini Sweden na Denmark.

Amesema mkutano huo ambao utajadili kwa ujumla vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu duniani hasa katika nchi za Magharibi unatazamiwa kufanyika Jumatatu ijayo ya Julai 31.

Tags