Iran yaishukuru OIC kwa kukubali kuitisha kikao cha kutetea Qur'ani Tukufu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa shukrani kwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa kukubali kuitisha kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa jumuiya hiyo kuhusu vitendo viovu vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden na Denmark.
Katika ujumbe wake wa Twitter siku ya Jumanne, Hossein Amir-Abdollahian alitoa shukurani zake kwa Katibu Mkuu wa OIC Hissein Brahim Taha na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanacvhama kwa kuafiki pendekezo la awali lililowasilishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq kwa ajili ya mkutano huo usio wa kawaida.
Katika ujumbe huo wa Twitter amesema: "Lengo letu la pamoja ni kuchukua hatua madhubuti ili kuzuia kurudiwa udhalilishaji dhidi ya Qur'ani Tukufu na maandiko mengine matakatifu." Naye msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani amesema mkutano huo unatarajiwa kufanyika tarehe 31 Julai.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya mkimbizi wa Iraq mwenye makazi yake Uswidi, anayetambuliwa kama Salwan Momika, kukivunjia heshima kitabu kitakatifu cha Waislamu.
Alifanya kitendo hicho cha kufuru kwanza mbele ya msikiti mkubwa kabisa wa Stockholm mwishoni mwa mwezi Juni, na kwa mara ya pili nje ya Ubalozi wa Iraq katika mji huo huo siku ya Alhamisi, huku kukiwa na ulinzi mkali uliotolewa na polisi wa Uswidi.
Na siku ya Ijumaa, wanachama wa kundi la Denmark lenye chuki na Uislamu, linaloitwa Danske Patrioter, waliinajisi Qur'ani Tukufu mbele ya Ubalozi wa Iraq katika mji mkuu wa Denmark, Copenhagen.
Siku ya Jumanne pia, kundi hilo dogo la mrengo wa kulia lilichoma moto nakala za Qur'ani Tukufu mbele ya balozi za Misri na Uturuki katika mji mkuu wa Denmark, katika kitendo kingine cha kufuru dhidi ya kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu.
Vitendo vya kufuru hiyo vimefungua milango ya maandamano katika ulimwengu wa Kiislamu, ikiwa ni pamoja na nchini Iran, huku nchi nyingi za Kiislamu zikilaani kitendo hicho.