Kumbukumbu za Tasua ya Imam Husain AS zafanyika kona zote za Iran
(last modified Fri, 28 Jul 2023 03:00:11 GMT )
Jul 28, 2023 03:00 UTC
  • Kumbukumbu za Tasua ya Imam Husain AS zafanyika kona zote za Iran

Jana Alkhamisi ilisadifiana na mwezi Tisa Mfunguo Nne, Muharram, siku ya maombolezo ya Tasua ya Imam Husain AS na mashahidi wengine wa mapambano ya Karbala ya mwaka 61 Hijria.

Maashiki na wapenzi wa Imam Husain AS katika kona zote za Iran ya Kiislamu, jana walishiriki katika maombolezo ya Tasua kwa hamasa kubwa zaidi kuliko miaka ya huko nyuma. 

Usiku wa Tasua pia, yaani usiku wa kuamkia jana Alkhamisi, Waislamu nchini Iran walishiriki kwa wingi katika kuadhimisha mapambano hayo na hasa mapambano ya Abbas bin Ali maarufu kwa jina la Abul Fadhl al Abbas, jemedari shujaa na nguzo muhimu mno ya Imam Husain AS ambaye baada ya kuuawa kwake kidhulma, maadui waliokuwepo kwenye jangwa la Karbala walitangaza kuwa wamemmaliza Imam Husain AS.

Jana Alkhamisi, waombolezaji katika kona zote za Iran walitangaza kwa sauti kubwa utiifu wao kwa wanamapambano wa Karbala na wajibari na na kujiweka mbali na maadui wa Uislamu na wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW.

Mkesha wa Tasua uliadhimishwa pia kwenye Husainia ya Imam Khomeini (MA) na kuhudhuriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Rais Ebrahim Raisi

 

Jana mchana, Rais Ebrahim Raisi akiwa pamoja na mawaziri wa serikali yake na idadi kubwa ya wafanyakazi, wakuu na wakurugenzi wa taasisi mbalimbali za Serikali aliungana na wananchi wengine katika Msikiti wa Salman Farsi hapa Tehran na kushiriki kwenye kumbukumbu za Tasua ya Imam Husain AS. 

Akihutubia waombolezaji, Rais Raisi alisema, kila mmoja leo hii anapaswa kushirki vilivyo katika vita vya haki dhidi ya batili kwa moyo imara, kwa muqawama kwa kujipinda kufanya kazi za maana na kwa jitihada za usiku na mchana ili kuwafikishia walimwengu uhakika wa njia ya haki iliyopiganiwa na Imam Husain AS.

Vile vile alisema, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni muendelezo wa Mapinduzi ya Imam Husain AS na kusisitiza kwamba, leo hii mfumo mpya wa kiutawala umo katika kujiunda duniani kwa baraka za damu toharifu za mashahidi wa dini tukufu ya Kiislamu.