Abdollahian: Iran na Afrika Kusini zina fursa nyingi za kupanua ushirikiano
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema, licha ya vikwazo vya upande mmoja na haramu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika fremu ya sheria za kimataifa, daima kuna fursa mbalimbali kwa Iran na Afrika Kusini za kupanua uhusiano.
Hussein Amir Abdollahian ambaye yuko Pretoria Afrika kushiriki katika mkutano wa 15 wa Kamisheni ya Ushirikiano ya Iran na Afrika Kusini amesema katika kikao cha pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naldi Pandor kwamba, Iran iko tayari kushirikiana kikamilifu na Afrika Kusini katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uga wa sayansi na teknolojia na kubadilishana ushirikiano katika nyanja za nishati na kadhalika.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema: Katika kikao cha kamisheni ya pamoja ya Iran na Afrika Kusini, wajumbe wa pamoja wa wizara, mashirika na taasisi za sekta ya umma na binafsi ya nchi hizo mbili walikuwa na mazungumzo muhimu na yenye tija kwa muda wa siku mbili, na kwamba, mazungumzo haya yalikuwa sehemu ya makubaliano na ramani ya njia ya ushirikiano wa pande mbili.
Kwa upande wake, Naldi Pandor, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afrika Kusini pia amesema: "Alifanya mazungumzo mazuri na ya kina kuhusu masuala ya pande mbili, kieneo na kimataifa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, na kwamba nchi hizo mbili zina misimamo ya pamoja katika masuala ya kimataifa.
Aidha Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afrika Kusini amesema, Pretoria na Tehran zinaunga mkono ushirikiano wa pande kkadhaa na kuthamini nafasi ya Umoja wa Mataifa kama taasisi ya pande kadhaa.