Raisi na Putin wasisitiza kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili na kimataifa
Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia wamefanya mazungumzo ya simu na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi, na Rais wa Shirikisho la Russia, Vladimir Putin, wamesisitiza azma ya nchi hizo mbili ya kustawisha zaidi uhusiano wa pande mbili katika nyanja za biashara, nishati, usafirishaji na mazingira.
Marais wa nchi hizo mbili pia wamejadili masuala yanayohusiana na ushirikiano katika masuala ya kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na uanachama kamili wa Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na hamu ya Iran kujiunga na kundi la BRICS.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jioni ya jana, Rais wa Russia, Vladmir Putin, alilaani shambulizi la kigaidi lililotokea kwenye haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Sayyid Ahmad bin Musa (Shah Cheragh) katika mji wa Shiraz nchini Iran na kutoa mkono wa pole kwa mwenzake wa Iran.
Jumapili iliyopita, gaidi kutoka Tajikistan alifyatua risasi katika haram ya Shah Cheragh, mjini Shiraz na kuua shahidi watu wawili. Watu wengine saba walijeruhiwa. Gaidi mmoja alikamatwa papo hapo na kukabidhiwa kwa vyombo vya sheria. Kundi la kigaidi la Daesh limedai kuhusika na shambulio hilo la kigaidi.
Iran na Russia zina maslahi ya kistratijia ya pamoja katika nyuga za pande mbili hususan uhusiano wa kiuchumi, kijeshi na kiusalama na pia masuala ya kieneo na kimataifa kama vile kukabiliana na sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani, na hilo limekuwa moja ya nguzo kuu za ushirikiano wa karibu kati ya Tehran na Moscow katika miaka ya hivi karibuni.