MSF yaonya: Mlipuko wa Ebola DR Congo ni wa kutisha sana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138772-msf_yaonya_mlipuko_wa_ebola_dr_congo_ni_wa_kutisha_sana
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limeonya kwamba mlipuko wa Ebola katika Mkoa wa Ituri nchini Kongo DR unaenea kwa kasi kubwa zaidi kuliko juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) ikifuatilia ongezeko la dharura ya afya ya umma sambamba na kuwepo mamia ya visa vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola.
(last modified 2026-05-31T12:48:09+00:00 )
May 31, 2026 12:45 UTC
  • MSF: Mlipuko wa Ebola huko Kongo unatisha
    MSF: Mlipuko wa Ebola huko Kongo unatisha

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limeonya kwamba mlipuko wa Ebola katika Mkoa wa Ituri nchini Kongo DR unaenea kwa kasi kubwa zaidi kuliko juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) ikifuatilia ongezeko la dharura ya afya ya umma sambamba na kuwepo mamia ya visa vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola.

MSF imeitaja hali ya mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa "ya kutisha sana" huku mamlaka za afya na timu za kibinadamu zikipambana kudhibiti mlipuko huo unaoenea kwa kasi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Alan Gonzalez, naibu mkurugenzi wa shughuli katika Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, amesema kwamba hali katika Mkoa wa Ituri imezorota sana wiki mbili tu baada ya mlipuko kutangazwa rasmi, akionya kwamba jamii na wafanyakazi wa afya walio mstari wa mbele wanakabiliwa na shinikizo kubwa.

Amesema, kasi ya maambukizi imeweka timu za kukabiliana na maambukizi katika mashinikizo makubwa, huku maambukizi yakijitokeza kwa kasi zaidi kuliko juhudi za kufuatiliwa na kudhibitiwa kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa MSF, visa vinavyoshukiwa vya Ebola vinatambuliwa kila siku, lakini uwezo mdogo wa upimaji unapunguza kasi ya utambuzi na kuchelewesha hatua za haraka za kukabiliana na ugonjwa.

Shirika hilo limeonya kwamba bila kupanuliwa haraka uwezo wa upimaji na udhibiti, mamlaka za afya zitakuwa katika hatari ya kupoteza udhibiti wa mwelekeo wa mlipuko wa Ebola.

Onyo hilo linakuja huku Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, akitembelea Mkoa wa Ituri ili kutathmini hali ilivyo.

WHO tayari imeainisha mlipuko wa Ebola nchini DRC na Uganda kama Dharura ya Afya ya Umma ya Wasiwasi wa Kimataifa, ikiangazia hatari zinazotokana na kuenea kwa virusi hivyo.

Kwa mujibu wa data za afya za Umoja wa Mataifa, zaidi ya visa 900 vinavyoshukiwa vimeripotiwa nchini DRC hadi sasa, ikiwa ni pamoja na vifo 223 vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola.