Raisi: BRICS inayaleta pamoja mataifa huru yanayopinga ubeberu
Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema Jumuiya ya BRICS ni nguvu mpya inayoinukia kwa kasi duniani, na ambayo imefanikiwa kuyaleta pamoja mataifa huru yanayotaka kuwa na ushirikiano wa kiuchumi na kukabiliana na ubeberu.
Aidha Rais Raisi amesema Jamhuri ya Kiislamu ina azma ya kuimarisha ushirikiano na BRICS ambayo inaundwa na nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Algeria, Argentina, Misri, Indonesia, Saudi Arabia, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi nyingi ziko mbioni kujiunga na kundi hilo lenye ushawishi mkubwa wa kiuchumi katika zama hizi za taathira za uchumi duniani.
Rais wa Iran amesema hayo usiku wa kuamkia leo hapa mjini Tehran, kabla ya kuondoka nchini kuelekea Afrika Kusini kwenda kushiriki mkutano wa kilele wa kundi la BRICS.

Mkutano huo wa jumuuiya ya nchi tano za BRICS pamoja na wakuu wa mataifa mengine yaliyoomba kujiunga na jumuiya hiyo ulianza mjini Johannesburg, Afrika Kusini juzi Jumanne, na unatazamiwa kumalizika leo.
Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, atafanya mazungumzo na maafisa wanaoshiriki mkutano huo mjini Johannesburg, kwa shabaha ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili na pande kadhaa na nchi zinazoshiriki mkutano huo.
Kundi la BRICS hivi sasa linakaribia kulipita Kundi la G7 kiuchumi na kwa mujibu wa tathmini, hisa ya nchi wanachama wa BRICS katika pato jumla la taifa itapindukia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.