Abdollahian: Tunataraji kuona uhalifu wa kivita dhidi ya Gaza ukikomeshwa haraka
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, tunataraji kuona uhalifu wa kivita dhidi ya Gaza ukikomeshwa haraka iwezekanavyo.
Akielezea wasiwasi wake kuhusu hali inayotawala katika eneo la Magharibi mwa Asia, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema: Tunataraji kuona uhalifu wa kivita dhidi ya Gaza huuko Palestina ukikomeshwa haraka iwezekanavyo.
Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo leo kabla ya kuondoka Jeddah Saudi Arabia kwa ajili ya kurejea nchini ambapo amezungumzia mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na matukio ya hivi karibuni katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina na kusema kuwa, wanachama wote wamekubaliana kwamba wanaharakati wa kisiasa hawapaswi kufumbia macho mauaji ya raia, wanawake na watoto na ni lazima wachukue hatua. Kadhalika Abdollahian amekosoa uwepo wa Rais Joe Biden wa Marekani katika eneo na uungaji mkono wake kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameashiria kuwepo kwa wasiwasi mkubwa katika anga ya kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na kuongeza kuwa: “Kila mtu ana wasiwasi na kuenea kwa vita, na bila shaka kwa hali ambayo sote tunaishuhudia, suala hili ni jambo lisiloepukika na tukio kama hilo linaweza kutokea saa yoyote."
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran pia amezungumzia madai ya kichekesho ya Wazayuni na Wamarekani kwamba hospitali hiyo ililengwa huko Gaza na Harakati ya Jihadul Islami na muqawama na kueleza kwamba, kujitokeza Marekani kwa nguvu zake zote za vyombo vya habari na kumuunga mkkono Netanyahu kuhusiana na jinai hiyo isiyo na mithili dhidi ya wagonjwa, hilo haliwezi kuusafisha uso mchafu wa Netanyahu na haiba yake ya kikatili.
Kabla ya hapo akizungumza katika mkutano wea dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) alisema kuwa, kuna udharura wa kupandishwa kizimbani viongozi wa utawala wa Kizayuni kutokana na jinai za kuchupa mipaka wanazozifanya dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.