Iran yataka jamii ya kimataifa ikabiliane na wahalifu wa Kizayuni
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamuri ya Kiislami ya Iran ameihutubu jamii ya kimataifa zikiwemo asasi za kimataifa, serikali na mataifa na kusema: "Simameni dhidi ya jinai za Kizayuni na waungaji mkono wao na muwatetee Wapalestina wanaodhulumiwa huko Ghaza kwa ajili ya amani na usalama wa dunia."
Katika kukabiliana na jinai za Wazayuni, vikosi vya muqawama vya Palestina vilianza operesheni ya "Tufani ya Al Aqsa" ukanda wa Ghaza dhidi ya ngome za utawala wa Kizayuni wa Israel kuanzia Jumamosi, Oktoba 7, 2023.
Tangu kuanza kwa operesheni hiyo, jeshi la Kizayuni, ambalo halina uwezo wa kukabiliana na wapiganaji wa muqawama, limekuwa likishambulia kwa mabomu maeneo ya raia, hospitali, vituo vya kidini na shule huko Ghaza.
Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Afya ya Palestina, zaidi ya watu 7,800 wameuawa shahidi na wengine takriban 20,000 wamejeruhiwa katika siku 21 za jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza.
Kuhusiana na jinai hizo za Wazayuni, "Nasser Kanani", Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, leo (Ijumaa) amehutubia jumuiya ya kimataifa yakiwemo mashirika ya kimataifa, serikali na mataifa katika mtandao wa kijamii wa X, akiiomba jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya wahalifu wa Kizayuni na waungaji mkono wao ili dunia iweze kushuhudia amani na usalama. "Simameni na muwatetee Wapalestina wanaodhulumiwa huko Ghaza."
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema: Iwapo jumuiya ya kimataifa zikiwemo asasi za kimataifa, serikali na mataifa hazitatoa jibu kali na la kuzuia jinai zote za kutisha ambazo zimekuwa zikifanywa na Wazayuni huko Ghaza katika kipindi cha wiki 3 zilizopita na wahalifu wa vita na wafuasi wao kubaki bila kuadhibiwa, basi mfumo wa kimataifa utapoteza itibari.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameendelea kusema: Kutochukuliwa hatua kali na kutokuadhibiwa Wazayuni watenda jinai za kivita huko Ghaza kunamaanisha kusalimu amri wapenda haki, wapigania uhuru na waungaji mkono wa amani na usalama wa dunia mbele ya watenda jinai za kivita na wahalifu wa kivita.