Raisi: Matukio ya Ghaza ni dhihirisho la vitendo visivyo vya kibinadamu
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyataja matukio ya Ghaza kuwa ni maonyesho ya kusikitisha ya vitendo vya kikatili na dhidi ya binadamu vinavyotekelezwa na utawala wa Kizayuni.
Mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni katika maeneo ya makazi ya Ukanda wa Ghaza yameingia wiki ya nne mfululizo, na kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Afya ya Palestina, zaidi ya Wapalestina 8,500 wameuawa shahidi, ambapo nusu yao ni watoto wasio na ulinzi na wanaodhulumiwa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Seyed Ibrahim Raisi ameyasema hayo katika kikao cha leo (Jumatano) cha baraza la mawaziri na kuongeza kwamba, matukio ya Ghaza ni dhihirisho la vitendo vya utawala haramu wa Kizayuni vilivyo dhidi ya ubinadamu, vikiwemo kuua watoto, kushambulia hospitali kwa kutumia mabomu yaliyopigwa marufuku na kuwazingira watu kila upande, na vile vile kuzuia utoaji wa misaada ikiwemo chakula na dawa katika eneo hilo. Amesema jinai hizo zinafanyika mbele ya macho ya jumuiya ya kimataifa.
Akisisitiza kuwa matukio ya Ghaza ni ishara tosha ya kushindwa jamii ya kimataifa katika kuimarisha usalama. Raisi ameongeza kuwa, mashambulizi ya kikatili yaliyotekelezwa na utawala haramu wa Israel jana Ghaza katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia ambapo damu ya watu wasio na hatia imemwangwa ni muendelezo wa jinai za kivita za utawala wa Kizayuni na jinai dhidi ya binadamu katika kipindi cha siku 20 zilizopita.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya nafasi ya moja kwa moja ya Marekani katika jinai hizo kupitia utoaji wa silaha na misaada ya kijeshi na uungaji mkono wa kisiasa kwa utawala wa Kizayuni. Aidha amesema jinai hizo zimedhihirisha kwamba mikataba mingi ya kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa imeshindwa kufanya kazi. Ameongeza kuwa ni muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kuangalia upya kanuni zilizopo.
Raisi amesema kura madhubuti ya nchi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kuidhinisha azimio la usitishaji vita huko Ghaza ndio sababu ya kutengwa Marekani katika jumuiya ya kimataifa. Aidha amesema hatua ya baadhi ya nchi za Magharibi ya kushirikiana na utawala wa Kizayuni katika mauaji ya watoto wachanga na jinai dhidi ya binadamu ni onyesho la unafiki, udanganyifu na undumakuwili katika mifumo ya kimataifa