Jeshi la Irani: Hii leo Gaza inashuhudia mauaji ya Holocaust ya kweli
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetangaza katika taarifa yake kwa mnasaba wa kuwadia siku ya leo ya tarehe 4 Novemba ambayo inajulikana hapa nchini kama siku ya Kupambana na Uistikbari kwamba, hii leo Gaza inashuhudiwa mauaji ya kweli na halisi ya Holocaust na mhusika mkuu ya mauaji ya watu madhulumu wa ardhi hii ni Marekani mtenda jinai.
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limesema katika taarifa yake kwamba, kuwadia Siku ya Mwenyezi Mungu ya tarehe 13 Aban (Novemba 4) ya kumbukumbu ya kutekwa kwa pango la ujasusi la Marekani (ubalozi wa Marekani) na vijana wanamapinduzi na werevu wa Iran ya Kiislamu, ni nukta ya mabadiliko katika historia inayong'ara ya Mapinduzi ya Kiislamu, ambayo ilikuwa na nafasi muhimu katika kukata mkono wa ubeberu na kuthibitisha na kuimarisha mfumo mtukufu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, chuki na uadui wa Marekani na taifa la Iran ni wa muda mrefu na jinai nyingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, zikiwemo mashambulizi ya moja kwa moja ya kijeshi, uchochezi na kuunga mkono utawala wa Baathi na makundi ya upinzani ya kisiasa, kuandaa makundi ya kigaidi, vikwazo vya kikatili, kuanzisha vita laini na kadhhalika ni mambo ambayo katu taifa letu halitasahau majeraha haya.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeashiria kile kinachojiri hivi sasa katika ukanda wa Gaza Palestina na kusema kuwa, kwa mara nyingine tena sura halisi ya unyama ya Uistikbari wa Dunia imedhihirika na hatua ya Marekani mtenda jinai ya kuunga mkono Israel inayofanya mauaji dhidi ya watoto imeweka wazi zaidi utambulisho wake halisi.
Tarehe 13 Aban 1358 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 4 Novemba 1979, wanafunzi wa Chuo Kikuu wa Iran walilivamia pango la kijasusi la Marekani mjini Tehran lililokuwa na ubalozi wa dola hilo la kibeberu baada ya kuongezeka njama za Marekani za kutaka kufanya mapinduzi mengine nchini Iran, siku hii inajulikana hhapa nchini kwa jina la Siku ya Mwanafunzi na Siku ya Kupambana na Uistikbari.