Iran yaunga mkono taarifa ya OIC inayolaani tishio la nyuklia la Israel
Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameunga mkono taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inayolaani vitisho vya utawala ghasibu wa Israelkuhusu kutumia silaha za nyuklia Ukanda wa Gaza.
Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ametuma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X akiunga mkono taarifa ya OIC iliyowasilishwa kwa Umoja wa Mataifa inayolaani tishio la viongozi wa utawala wa Israel kuhusu kutumia silaha za nyuklia Ukanda wa Gaza. Taarifa ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu iliyotolewa tarehe 6 Novemba, imeeleza kuwa jumuiya hiyo inautaka utawala ghasibu wa Israel uache kumiliki silaha za maangamizi umati na ujiunge na mkataba wa NPT na kukubali kukaguliwa na kusimamiwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ta Atomiki (IAEA).
Sehemu moja ya ujumbe huo wa pamoja wa nchi wanachama wa OIC kuhusu tishio la utawala wa Israel la kutumia silaha za nyuklia imeeleza kuwa: Misimamo ya kushangaza ya Israel kuhusu kutumia silaha za nyuklia dhidi ya wananchi wa Palestina huko Ukanda wa Gaza inalaaniwa; na kwamba Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu inaamini kuwa matamshi hayo ya chuki ya afisa wa Israel yana lengo la kueneza fikra za kibaguzi za kigaidi na inalaani matamshi hayo na kuitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua madhubuti ili kusitisha uvamizi wa kijeshi, mauaji ya kila uchao na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa unaofanywa na Israel.
Itakumbukwa kuwa Amikhai Eliyahu, Waziri wa Turathi za Utamaduni wa utawala wa Kizayuni siku kadhaa zilizopita alisema kuwa, utumiaji wa mabomu ya nyuklia huko Ghaza ndio suluhisho pekee linalowezekana na kwamba vita vinagharimu pesa kwa watekaji nyara.
Mashambulizi ya kila siku huko Ukanda wa Gaza na kuuliwa wanawake na watoto wa Kipalestina yanaendelea katika hali ambayonchi za Magharibi zinazouunga mkono na kuusaidia kwa hali na mali utawala wa Kizayuni hadi sasa zimeyapigia kura ya veto maazimio yote ndani ya Baraza la Usalama la UN yanayotaka kusitishwa vita Ukanda wa Gaza. Nchi hizo za magharibi zinafanya kila ziwezalo ili kupasisha maazimio ya kuiunga mkono pakubwa Tel Aviv badala ya kufanya juhudi za kusitisha mauaji na mashambulizi ya mabomu dhidi ya raia wa Palestina wa Ukanda wa Gaza.