Raisi: Damu za mashahidi wa Palestina zitaleta nidhamu ya dunia yenye uadilifu
(last modified Sun, 19 Nov 2023 14:36:45 GMT )
Nov 19, 2023 14:36 UTC
  • Raisi: Damu za mashahidi wa Palestina zitaleta nidhamu ya dunia yenye uadilifu

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema 'nidhamu mpya ya dunia yenye uadilifu' itaibuka kutokana na damu za wananchi wa Palestina zilizomwagwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vyake vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Rais Raisi amesema hayo leo Jumapili katika kaunti ya Shahriar mkoani Tehran na kuongeza kuwa, watu katika pembe mbalimbali za dunia wanauchukia utawala wa Kizayuni, na pia wameghadhabishwa na utendaji mbovu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo, kwa kushindwa kusimamisha jinai za Israel dhidi ya Wapalestina.

Sayyid Raisi amesema, "Hii leo, watu wanahisi kuna udharura wa kuundwa mfumo mpya wa nidhamu ya dunia yenye uadilifu. Hakuna shaka nidhamu ya dunia yenye uadilifu itaundwa kutokana na irada ya mataifa na damu toharifu ya Wapalestina."

Rais wa Iran ameeleza bayana kuwa, kusimama kidete wananchi wa Palestina kumeipa dunia nzima somo la kupambana na kutangaza bayana chuki zao dhidi ya maadui wa jamii ya mwanadamu.

Jinai za Wazayuni kwa watoto na wanawake wa Gaza

"Damu toharifu ya watoto 5,000 wa Kipalestina italeta kisasi kitakatifu ambacho kitawapiga Mafarao wa enzi hizi na kuhitimisha utawala wao." ameeleza Sayyid Raisi.

Tokea Oktoba 7, utawala ghasibu wa Israel umeendelea kulenga maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza, hususan majengo ya makazi na hospitali, na matokeo yake yamekuwa ni kuuawa shahidi zaidi ya Wapalestina 12,000, ambapo 5,000 kati yao wakiwa ni watoto na 3,300 wanawake.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, takriban Wapalestina 30,000 wamejeruhiwa, asilimia 70 kati yao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo katika kipindi cha siku 43.