Nov 23, 2023 03:07 UTC
  • Eslami: IAEA iache kuingiza siasa kwenye kesi ya Iran

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) ameutaka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ujiepushe na tabia ya kuingiza siasa kwenye faili la nyuklia la Jamhuri ya Kiislamu.

Mohammed Eslami alisema hayo jana Jumatano katika kikao na waandishi wa habari pambizoni mwa mkutano wa Baraza la Mawaziri hapa Tehran na kuongeza kuwa, Iran imeruhusu wakaguzi 120 wa taasisi hiyo ya nyuklia ya Umoja wa Mataifa waingie nchini.

Aidha ameashiria uamuzi wa Iran wa kutoruhusu baadhi ya wakaguzi hao kuingia hapa nchini na kusema: Kwa mujibu wa Kipengee cha 9 cha Hati ya IAEA, Iran ina haki ya kukubali au kukataa wakaguzi waingie nchini.

Eslami amesisitiza kuwa, maingiliano chanya na ushirikiano baina ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki haupaswi kuathiriwa na mashinikizo ya kisiasa.

Kadhalika amekosoa mienendo ya nchi za Magharibi ya kuutumia vibaya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuishinikiza Iran.

Eslami (kushoto) alipokutana na Rafael Grossi, Mkuu wa IAEA hapa Tehran

IAEA chini ya mashinikizo ya Wamagharibi, ilidai kuwa hatua ya Iran kutoruhusu baadhi ya wakaguzi wake kuingia nchini mnamo Septemba iliathiri utendaji kazi wa taasisi hiyo ya UN.

Wakala wa IAEA mara kadhaa umekuwa ukitoa madai kuhusu shughuli za amani za kuzalisha nishati ya nyuklia za Iran chini ya mashinikizo ya pande za Magharibi na utawala haramu wa Israel, lakini madai hayo hayawiani na rekodi za ushirikiano kati ya Iran na Wakala huo. 

Eslami ameongeza kuwa, Iran itaendeleza uhusiano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ndani ya fremu ya kanuni husika na itazuia hali ya kutoelewana katika mchakato wa ushirikiano wa Iran na wakala huo.

Tags