Kiongozi Muadhamu; kushindwa Wazayuni hakutafidiwa kwa jinai
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika kikao na washindi wa nishani za Michezo ya Asia na Para-Asia huko Hangzhou na wanamichezo wengine wa Iran kuwa, mienendo yao ya heshima katika medani za michezo ni dhihirisho la sura ya taifa la Iran, na kusema kuhusu matukio ya Gaza kuwa utawala wa Kizayuni, pamoja na jinai zake zote, haujaweza na wala hautaweza kufidia kushindwa kwake kukubwa kwake hivi karibuni na katika mustakbali.
Ayatullah Khamenei katika sehemu ya matamshi yake katika kikao hicho kilichofanyika Jumatano ameelezea kwa mukhtasari matukio ya hivi karibuni ya Gaza kwa namna ya tafsiri ya kimichezo na kusema: Utawala wa Kizayuni ulipata pigo la kiufundi katika operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa huko Gaza wakati ambapo Hamas ambayo si serikali wala nchi yenye uwezo, bali ni kundi la wanamapambano tu, limeweza kutoa pigo kubwa kwa utawala ghasibu wa Kizayuni ambao una suhula na zana nyingi kupita kiasi. Huku akisisitiza kuwa fedheha kubwa ya utawala wa Kizayuni haitafidiwa na jinai hizo, amesema: Wafahamu kwamba ukatili huo hautapita bila jibu na hujuma na mashambulizi ya mabomu yatafupisha umri wa utawala huo ghasibu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hapo awali pia alitaja tukio la kushindwa utawala wa Kizayuni huko Gaza kuwa tukio la kweli na kusisitiza kuwa utawala huo hadi sasa haujaweza kushinda huko Gaza na hautapata kushinda katika siku zijazo. Ni wazi kuwa kutokana na muqawama wa wananchi wa Palestina baada ya siku 47 hatimaye Jumatano utawala wa Kizayuni ulikubali kusimamisha vita kwa muda huko Gaza na kukubali masharti ya Hamas baada ya kutenda jinai nyingi katika eneo hilo. Usitishaji vita huo wa muda umefikiwa wakati ambapo hapo awali Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, alikuwa akikataa makubaliano yoyote akidai kuwa utawala huo utauteka Ukanda wa Gaza katika kipindi kifupi. Maghasibu hao pia walikuwa wakidai kwamba watayatokomeza makundi ya Hamas na Jihadul Islami katika kipindi cha siku 10. Kwa mujibu wa makubaliano ya usitishwaji vita, pande mbili zinazopigana zitasimamisha mapigano, na pia kusimamisha harakati zote za kijeshi za utawala wa Kizayuni katika maeneo yote ya Gaza ikiwa ni pamoja na kusimamishwa shughuli za kupiga doria magari ya kijeshi ya utawala huo katika maeneo hayo. Pia mateka 50 wa Kizayuni wataachiliwa huru mkabala wa kuachiliwa huru wanawake na watoto 150 wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za kuogofya za Wazayuni kwa miaka 19 sasa.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utawala wa Kizayuni haujajipatia mafanikio yoyote, kwa sababu umelazimika kukubali masharti ya muqawama ya kusimamisha mashambulizi ya kijeshi bila ya kuachiliwa huru wafungwa wote wa Kizayuni. Hii ni pamoja na kuwa hadi kufikia hatua hii utawala wa Kizayuni umepata hasara kubwa za kijeshi, kisiasa na kiuchumi. Kwa upande wa ndani pia, Netanyahu ndiye mtuhumiwa wa kwanza wa kushindwa katika operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, na wala hakuweza kuiteka Gaza na kuangamiza Hamas. Kuongezeka vifo vya Wazayuni pia kumefanya hali kuwa ngumu kwa ajili ya kuendelea vita huko Gaza. Kwa mfano, katika muda wa saa 48 zilizopita za mapigano, wanajeshi, maafisa na makamanda 30 wa Kizayuni waliuawa akiwemo Tamir Yedai, kamanda wa tawi la 298 la Brigedi ya Jeshi la Kizayuni.
Aidha mashinikizo ya waliowengi ulimwenguni dhidi ya kusimamishwa jinai za Wazayuni na pia kuwaunga mkono Wapalestina yanazidi kuongezeka kwa kiasi kwamba hata katika nchi waitifaki wa utawala huo zikiwemo Marekani na Uingereza kila siku maandamano ya kuunga mkono taifa la Palestina yanaendelea kuongezeka. Kwa upande mwingine, hali ya kiuchumi ya utawala wa Kizayuni nayo iko katika hali mbaya zaidi kihistoria. Sekta ya utalii ya utawala huo imeharibika kabisa na kukimbia Wazayuni pia kumepelekea kufungwa biashara nyingi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Kwa hivyo, utawala wa Kizayuni si tu kwamba umeshindwa kufikia malengo yake katika vita vya Gaza na kupata hasara kubwa katika nyanja zote za kisiasa, kijeshi na kiuchumi, bali pia hivi sasa umekiri kushindwa tena katika vita hivyo kwa kukubali masharti ya wanamuqawama wa Palestina. Katika kikao na wanamichezo hao, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiashiria kushindwa Wazayuni kujiondoa katika mashinikizo, aibu na fedheha ya kushindwa huko ameongeza kuwa: Wanaonyesha nguvu zao katika hospitali na shule za Gaza, lakini kazi hii ni sawa na ya mwanariadha ambaye ameshindwa uwanjani, lakini analipiza kisasi kwa kuwashambulia mashabiki wa timu ya upinzani, kwa kuwatukana na kuwapiga.
.