Onyo la Iran kuhusu uingiliaji wowote wa Marekani katika mustakabali wa Gaza
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, uamuzi kuhusu mustakbali wa Ukanda wa Gaza uko mikononi mwa wakazi wake na kuwa uingiliaji wowote wa Marekani katika uwanja huo utashindwa tu.
Katika mazungumzo yake ya simu siku ya Jumapili na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki, Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa mustakabali wa watu wa Gaza unapaswa kuainishwa kupitia Hamas, kama serikali halali inayotambulika katika eneo hilo, na kuwa Marekani haina haki yoyote ya kuingilia maamuzi ya watu wa Gaza.
Kwa kuzingatia kuwa leo ni siku ya nne na ya mwisho ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda kati ya Hamas na utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu amesema katika mazungumzo ya simu na Rais Joe Biden wa Marekani kuwa mashambulizi katika Ukanda wa Gaza yataanza tena baada ya kumalizika kwa usitishaji vita na kusisitiza kuwa anakaribisha pendekezo la kurefushwa usitishaji vita iwapo litadhamini kuachiliwa mateka wa Kizayuni.
Katika mazungumzo hayo ya simu, Rais wa Marekani amedai kuwa, pendekezo la kubuniwa madola mawili ndiyo njia pekee ya kuwahakikishia Wazayuni na Wapalestina usalama wa muda mrefu, na kuwa Marekani bado inatilia mkazo jambo hilo.
Ingawa viongozi wa Marekani na wa utawala wa Kizayuni wanajiepusha kuweka wazi sera na siasa zao kuhusu Gaza, baada ya operesheni ya Oktoba 7 ya vikosi vya Hamas na mashambulizi ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni katika ukanda huo, lakini tunaweza kukisia maamuzi na sera zao kupitia matamshi wanayotoa na vile vile ripoti za vyombo vya habari.
Watawala wa Kizayuni wanasema hawana nia ya kuikalia kwa mabavu Gaza, lakini wakati huohuo wanasema hawakubaliana na suala la kuendelea utawala wa Hamas huko Gaza baada ya shambulio la Oktoba 7.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken amesema: Serikali ya Hamas haiwezi kuendelea kuitawala Gaza na pia hatuwezi kuikabidhi Israel usimamizi wa Gaza kama wanavyopendekeza.
Matamshi hayo yanaonyesha kuwa, Marekani muhimili mkuu wa kuendelea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza, inachunguza mapendekezo kadhaa kuhusu mustakbali wa eneo hilo kama vile kusimamiwa masuala ya Ukanda wa Gaza na Mamlaka ya Utawala wa Ndani ya Palestina, utawala muda chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, kutumwa vikosi vya kulinda amani eneo la Gaza au kukabidhiwa usimamizi wa huo kwa baadhi ya nchi za Kiarabu waitifaki wa Magharibi.
Nukta muhimu na ya pamoja katika chaguzi zote hizo ni kuondolewa Hamas madarakani na kupuuzwa haki ya Wapalestina ya kujiamulia hatima yao wenyewe, ambapo harakati ya Hamas ni mhimili wa muqawama na fikra iliyokita mizizi katika nyoyo za Wapalestina, na haitaweza kufutwa hata baada ya kumalizika vita vya Gaza, bali imekuwa ikipata umaarufu siku baada ya yingine. Uchunguzi wa kituo cha utafiti cha Orad, ambao matokeo yake yalichapishwa na kanali ya 12 ya Kizayuni, unaonyesha kuwa kutokana na vita hivyo, uungaji mkono kwa Hamas sasa uko katika kiwango cha juu zaidi katika Ukanda wa Gaza na hata Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ambapo asilimia 90 ya waliohojiwa wametangaza ungaji mkono wao mkubwa kwa harakati hiyo.
Ukweli ni kwamba mazungumzo ya miongo saba ya Wapalestina na juhudi eti za kutafuta amani, zilizopelekea mapatano ya Camp David na Oslo hayakuwa na matokeo yoyote ya maana kwa Wapalestina na muqawana ndilo chaguo pekee la kukabiliana na siasa za kujitanua za Wazayuni. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mapatano hayo yamepelekea Wapalestina kunyumwa haki yao ya kimsingi ya kujitawala, bali pia yameandaa uwanja wa Wazayuni kupora ardhi zao na wakati huo huo kutekeleza jinai za kutisha dhidi yao.
Kwa mantiki hiyo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuunga mkono muqawama wa Wapalestina wa kutaka kurejeshwa ardhi zao na vilevile kutambuliwa rasmi uhalali wa serikali ya Hamas iliyoingia madarakani kwa kura za wananchi, amelaani uingiliaji wowote wa Marekani kuhusiana na mustakabali wa Gaza na kuutaja kuwa ni mwendelezo wa jinai za nchi hiyo dhidi ya Wapalestina.