Dec 14, 2023 02:41 UTC
  • Eslami: Maadui wameshindwa kuzuia ustawi wa sekta ya nyuklia ya Iran kwa vikwazo

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema maadui wameshindwa kuzima ustawi wa mradi wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu wenye malengo ya amani kupitia vikwazo haramu.

Kwa mujibu wa Press TV, Mohammed Eslami alisema hayo jana Jumatano na kuongeza kwamba, "AEOI ina jukumu la kistratejia la kuzalisha nishati kwa ajili ya nchi hii. Hakuna shaka maadui wamejaribu kuzuia ustawi wa Iran kupitia vikwazo, lakini wamefeli."

Eslami amesema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kampuni ya Chuma ya Mobarakeh mkoani Isfahan, katikati ya Iran na kueleza bayana kuwa, AEOI imeazimia kuzalisha kilowati 20,000 za nishati ya nyuklia kufikia mwaka 2041.

Mkuu huyo wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amebainisha kuwa, sababu kuu ya vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ni kuvunja mori na moyo wa kujiamini wa wananchi wa Iran.

Mhandisi Eslami vilevile amesema, kama Iran isingekuwa na teknolojia ya nyuklia, isingeweza kutoa matibabu kwa kutumia teknolojia hiyo ambayo faida zake kuu ni za kimatibabu.

Ameongeza kuwa, licha ya kuweko vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa Tehran, lakini taifa hili la Kiislamu halijavunjika moyo kabisa, bali limejipinda kufanya utafiti wa kina wa sekta mbalimbali na limefanikiwa kuwa na uwezo imara na wa kujitegemea wa kuunganisha teknolojia na uzalishaji bidhaa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imegeukia matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia kwa kutegemea uwezo wa wataalamu wa ndani na imethibitisha kwa nia njema kwamba haina malengo mengine isipokuwa matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia; na kwa msingi huo imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

 

Tags