Apr 18, 2024 13:30 UTC
  • SEPAH: Vitisho vya Israel dhidi ya Iran si vipya na Tehran muda wote iko tayari kujibu mashambulizi ya adui

Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran SEPAH amesema kuwa, vitisho vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran haviwezi kuifanya Jamhuri ya Kiislamu kubadilisha sera na siasa zake kuhusu kustafidi kwa njia ya amani na teknolojia ya nyuklia.

Brigedia Jenerali Ahmad Haq Talab, Kamanda wa Jeshi la SEPAH katika suala la kulinda usalama wa vituo vya nyuklia vya Iran amesema kuwa, vitisho vilivyotolewa na utawala wa Kizayuni baada ya shambulizi la kulipiza kisasi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya Israel si vya leo wala jana, bali vimekuwepo kwa miaka mingi na utawala huo umeshafanya mara kadhaa mashambulizi ya kigaidi ya kujaribu kukwamisha shughuli za nyuklia za Iran lakini Jamhuri ya Kiislamu iko imara katika kustafidi na teknolojia hiyo muhimu. 

Amesema, kwa mujibu wa sheria zote za kimataifa, ni marufuku kushambulia taasisi za nyuklia za eneo lolote lile, lakini pamoja na hayo utawala wa Kizayuni haujali sheria za kimataifa na ndio maana muda wote Jamhuri ya Kiislamu imejiandaa kikamilifu kukabiliana na vitisho vya utawala huo pandikizi.

Kituo cha nyuklia cha Dimona cha utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Ameongeza kuwa, vikosi vya ulinzi vya Iran vina taarifa za kutosha kuhusu vituo vya nyuklia vya adui Mzayuni na iwapo Israel itafanya upuuzi wowote dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran hapo hapo Tehran itashambulia vituo vya nyuklia vya utawala wa Kizayuni na kwamba makombora ya Iran yako tayari-tayari yanasubiri kufyatuliwa tu. 

Kwa mara nyingine amesisitiza kuwa, kama utawala wa Kizayuni wa Israel utafanya shambulio lolote lile dhidi ya vituo na taasisi za nyuklia za Iran, bila ya shaka yoyote itapata majibu makali zaidi kutoka kwa Iran tena kwa kutumia silaha kali zaidi.

Tags