Dec 15, 2023 02:58 UTC
  • Maspika wa mabunge ya Iran na Algeria wasisitiza kusitishwa jinai za Wazayuni Ukanda wa Gaza

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ametangaza utayarifu wa Bunge la Iran kufanya kikao cha dharura cha Kamati ya Kudumu ya Palestina katika ngazi ya maspika wa mabunge ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kuchunguza njia za kivitendo za kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.

Akizungumza kwa njia ya simu na Spika mwenzake wa Bunge la Algeria, Ibrahim Boughali, Spika Mohammad Baqer Qalibaf, ameashiria ukatili unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel na mauaji yake dhidi ya Wapalestina hususan wanawake na watoto wanaodhulumiwa katika Ukanda wa Gaza na kusema: Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran limejiandaa kikamilifu kuitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Kudumu ya Palestina katika ngazi ya maspika wa mabunge ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kuchunguza njia za kivitendo za kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.

Spika wa Bunge la Iran amepongeza misimamo na nafasi ya Algeria katika kulaani jinai za utawala ghasibu wa Israel na juhudi za Bunge la nchi hiyo za kuwahami na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na akasema, jumuiya za kimataifa na nchi nyingi zimelaani mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni na katika kikao cha hivi karibuni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia lilitoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano, lakini Marekani ilipinga suala hilo na kuunga mkono jinai za Israel. 

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Algeria pia amepongeza misimamo madhubuti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutetea na kuunga mkono kadhia ya taifa la Palestina na kusema kuwa, ingawa damu nyingi za watu wasio na hatia zimemwagwa katika vita vya Gaza, na hospitali nyingi, makanisa, misikiti na nyumba zimeharibiwa, lakini malengo ya ukombozi wa Wapalestina yamerudi kwenye nafasi yake. 

Akiashiria hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel kabla ya vita vya Gaza, Ibrahim Boughali amesema, inasikitisha kwamba, baadhi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu zilijaribu kuboresha uhusiano wao na utawala huo kwa namna ambayo ingewasahaulisha walimwengu kadhia ya ukombozi wa Palestina licha ya kujua vyema jinai na ukatili unaofanywa na utawala huo unaoua watoto wadogo; lakini hivi sasa nchi za Ulaya na nchi nyingi za Amerika ya Kusini zinalaani mienendo ya kinyama ya utawala wa Kizayuni, na zimepiga marufuku hata uagizaji wa bidhaa kutoka Israel; na hili ni suala jingine chanya la Muqawama wa watu wa Gaza.

Spika wa Bunge la Algeria amekosoa mienendo ya Marekani ya kuiunga mkono Israel na kuongeza kuwa, watu wa dunia wanalaani na kupinga vikali tabia hiyo ya kinyama ya Marekani na wasisitiza ulazima wa kusitishwa mauaji ya kimbari ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.

Tags