Iran: Haiwezekani kabisa kuuvunja nguvu muqawama
(last modified Wed, 20 Dec 2023 11:14:56 GMT )
Dec 20, 2023 11:14 UTC
  • Iran: Haiwezekani kabisa kuuvunja nguvu muqawama

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, harakati ya muqawama ni uhakika wa kieneo ambao ndio unaoleta utulivu na usalama katika ukanda huu mzima na ndiyo nguvu inayopambana kikweli na vitendo vya kigaidi na magenge ya ukufurishaji.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Ali Baqeri Kani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa amesema hayo leo mjini Tokyo Japan kwenye ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu katika kikao maalumu kilichohudhuriwa na wanafikra 70 wa Japan akisisitiza kuwa, hivi sasa Marekani inang'ang'ania siasa zake za kiistakbari za kuifanya dunia kutawaliwa na kambi moja kwani haitaki kupatikane uadilifu ulimwenguni. 

Amesema, uzoefu unaonesha kuwa, siasa za kibeberu za Marekani katika makhusiano ya kimataifa ndizo zinazohatarisha usalama wa dunia nzima na kukwamisha kupatikana utulivu wa kudumu, wakati mtazamo wa Iran kupigania haki na kuhakikisha kila taifa linapewa haki linayostahiki katika uhusiano wa kimataifa, ndiyo fikra ya kudumisha amani na utulivu ulimwenguni.

Harakati za muqawama wa Kiislamu

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, kustawi kwa haraka fikra ya kuweko kambi kadhaa duniani ni ushahhidi kwamba mataifa ya dunia yameelewa kuwa mfumo wa kambi moja ni wa kidhalimu na si kitu cha kudumu wakati mfumo wa kambi kadhaa unatoa hakikisho la kudhaminiwa mahitaji makuu ya mataifa ya dunia yaani kuweko uadilifu na kila taifa kupata haki yake.

Mwezi Agosti mwaka huu pia, Baqeri Kani alisema kuwa, jinai za Israel za kuuaa watoto wa Kipalestina zimekuwa ni jambo la kawaida kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, na kwamba umwagaji damu huo unadhihirisha wazi kuwa Wazayuni wanakiogopa mno kizazi kipya cha Wapalestina.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran alisisitiza pia kuwa, Palestina itaendelea kuwa kadhia kuu ya umma wa Kiislamu, huku akitoa mwito kwa serikali za Kiislamu kuimarisha uungaji mkono wao kwa Wapalestina katika nyuga zote.