Jumapili, 08 Disemba, 2024
Leo ni Jumapili, 6 Mfunguo Tisa Jamad al-Thani 1446 Hijria sawa na 08 Disemba, 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, ulianguka utawala wa Washugani au kwa jina jingine watawala wa kijeshi huko Japan. Kuanguka kwa utawala huo kulipelekea kuanza kwa marekebisho ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni nchini humo. Washugani walikuwa moja kati ya makumi ya silsila zenye nguvu huko Japan, walioanzisha utawala wao wa kidikteta tangu karne ya 12 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 121 aliaga dunia Herbert Spencer mwanafikra na mwanafalsafa wa Kiingereza. Spencer alizaliwa mwaka 1820 na kujifunza elimu mbalimbali kutoka kwa baba yake. Alijiongezea ujuzi na elimu kutokana na juhudi zake za kupenda kutalii mambo mbalimbali. Herbert Spencer aliamini kuwa, mtu anaweza kujipatia elimu kwa kushuhudia na kupata uzoefu.

Miaka 110 iliyopita katika siku kama ya leo, vilijiri vita vya baharini vya Falkland pambizoni mwa visiwa vya Falkland katika Bahari ya Atlantic kati ya Uingereza na Ujerumani. Vikosi vya wanamaji vya Ujerumani vilipigwa vibaya na vile vya Uingereza na visiwa hivyo vikatwaliwa tena na Waingereza. Visiwa vya Falkland ambavyo Argentina inasema ni milki yake, bado vinakaliwa kwa mabavu na Waingereza.

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, Chian Kai-shek kiongozi wa wapigania uhuru wa China alikimbilia Taiwan akiwa na wafuasi wake wengi baada ya kushindwa na wapiganaji wa chama cha Kikomonisti chini ya uongozi wa Mao Tse Tung na akaunda serikali ya kitaifa ya Uchina. Uungaji mkono wa Marekani kwa kiongozi huyo wakati huo ulipelekea Taiwan kujitenga na Uchina na kiti cha nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kikatolewa kwa Taiwan. Hata hivyo mwaka 1971, kufuatia mazungumzo kati ya China na Marekani, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitambua Jamhuri ya Watu wa China kwa kura nyingi, na nchi hiyo ilikubaliwa katika Baraza la Usalama, na hivyo Taiwan ikapokonywa uanachama katika Umoja wa Mataifa.

Miaka 33 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti na kuutangaza utawala wa Baath wa Iraq kuwa ndio ulioanzisha vita vya miaka minane dhidi ya Iran. Katika siku hiyo, Javier Perez de Cuellar Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa alitangaza katika ripoti yake kuwa Iraq iliivamia Iran tarehe 22 Septemba mwaka 1980. Miji na vijiji vingi vya mpakani mwa Iran vilitekwa na kukaliwa kwa mabavu huku wanawake, watoto na wanaume wengi wakiwa wahanga wa vita hivyo vikubwa katika uvamizi huo ambao uliungwa mkono kwa hali na mali na nchi za Magharibi.
