Rais Raisi amwambia Amir wa Kuwait: Palestina ni kadhia nambari moja
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106242-rais_raisi_amwambia_amir_wa_kuwait_palestina_ni_kadhia_nambari_moja
Huku kukiwa na vita vya mauaji ya halaiki vinavyoendelea vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, Rais Ebrahim Raisi wa Iran amelitaja suala la Palestina kuwa suala "muhimu zaidi" la Asia Magharibi na dunia nzima.
(last modified 2023-12-21T02:46:24+00:00 )
Dec 21, 2023 02:46 UTC
  • Rais Raisi amwambia Amir wa Kuwait: Palestina ni kadhia nambari moja

Huku kukiwa na vita vya mauaji ya halaiki vinavyoendelea vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, Rais Ebrahim Raisi wa Iran amelitaja suala la Palestina kuwa suala "muhimu zaidi" la Asia Magharibi na dunia nzima.

Rais wa Iran aliyasema hayo katika mazungumzo ya simu Jumatano na Amir wa Kuwait Sheikh Mishal Al Ahmad Al Jaber Al Sabah.

Raisi ameongeza kwamba,"Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kushirikiana na nchi nyingine katika kurejesha haki halali za taifa la Palestina."

Utawala katili wa Israel ulianzisha vita hivyo tarehe 7 Oktoba kufuatia operesheni iliyofanywa na harakati za Kiislamu za kupigania ukombozi wa Palestina huko Gaza. Zaidi ya watu 20,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuawa kinyama tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya eneo hilo.

Pia siku ya Jumatano, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala katili wa Israel alifutilia mbali matarajio ya kusitishwa mapigano yoyote katika Ukanda wa Gaza, akidai kuwa utawala huo utaendeleza vita hadi "malengo" yake yote yatimizwe.

Waziri Mkuu wa utawala katili wa Israel Benjamin Netanyahu

Katika mazungumzo hayo ya simu, Rais wa Iran ametoa shukurani zake kwa Amir wa Kuwait kutokana na uungaji mkono wa nchi yake kwa haki za taifa la Palestina, na kupinga kwake mchakato wa kuanzisha uhusiano na "utawala haramu na ghasibu wa Kizayuni."

Kwingineko katika matamshi yake, Raisi amesema sera ya Jamhuri ya Kiislamu imejikita katika uimarishaji na upanuzi wa uhusiano na nchi jirani.

Katika muktadha huo huo, Rais wa Iran amesisitiza kuwa ushirikiano na maelewano kati ya majirani ndio njia pekee ya kutatua masuala ya kieneo na kubaini kuwa uwepo wa madola ajinabi katika eneo hili ni chanzo cha matatizo.

Kwa upande wake, Amir wa Kuwait amesema msimamo wa nchi yake kuhusu haja ya kurejeshwa haki za Wapalestina hauwezi kubadilika.

Ameonyesha matumaini kwamba matatizo ya kikanda yatatatuliwa haraka iwezekanavyo kwa amani, na kuwa utulivu na usalama utaenea katika eneo lote la Asia Magharibi.