Raisi: Ulimwengu umeshangazwa na mapambano ya Wapalestina dhidi ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106278-raisi_ulimwengu_umeshangazwa_na_mapambano_ya_wapalestina_dhidi_ya_israel
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema dunia inashangazwa na Muqawama na mapambano ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala wa haramu wa Israel.
(last modified 2023-12-22T00:51:07+00:00 )
Dec 22, 2023 00:51 UTC
  • Raisi: Ulimwengu umeshangazwa na mapambano ya Wapalestina dhidi ya Israel

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema dunia inashangazwa na Muqawama na mapambano ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala wa haramu wa Israel.

Akihutubia umati mkubwa wa watu katika mji wa kaskazini mwa Iran wa Gorgan jioni ya Alhamisi jana, Rais Ebrahim Raisi alipongeza Muqawama na mapambano ya Wapalestina huko Gaza katika kukabiliana na mashambulizi ya zaidi ya miezi miwili ya Israel na kusema: Dunia nzima inashangazwa na nguvu na azma ya vijana wa Kipalestina. Ameongeza kuwa wakuu wa nchi nyingi wanakiri rasmi kuhusu ushujaa wa vijana hao na wanashangaa ni vipi Wapalestina wameweza kusimama kidete katika ardhi inayotajwa kuwa jela kubwa zaidi ya wazi duniani!

"Muqawama na mapambano haya yamechochewa na nguvu isiyoshindwa ya watu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tunaamini kwamba damu inashinda upanga", amesisitiza Sayyid Ebrahim Raisi. 

Wapiganaji wa Hamas

Utawala ghasibu na vamizi wa Israel ulianzisha vita dhidi ya watu wa Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya kundi la wapigania ukombozi la Hamas kutekeleza operesheni ya kushangaza ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala huo ili kukabiliana na ukatili wa Israel huko Palestina.

Tangu kuanza kwa mashambulizi hayo yanayoungwa mkono na Marekani, utawala ghasibu wa Israel umeua zaidi ya Wapalestina 20,000 wakiwemo watoto 8,000 na wanawake 6,200 na kuwajeruhi wengine 52,586. Maelfu zaidi wametoweka na inakisiwa kuwa wameaga dunia chini ya vifusi vya nyumba zilizoharibiwa kwa makombora ya jeshi la Israel.