Jeshi la Wanamaji la Iran lapokea makombora mapya ya cruise
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106376-jeshi_la_wanamaji_la_iran_lapokea_makombora_mapya_ya_cruise
Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limepokea mfumo wa kimkakati wa makombora ya cruis wa Talayieh na mfumo wa makombora wa Nasir na hali kadhalika helikopta za kwanza za vita vya kieletroniki na kijasusi.
(last modified 2023-12-24T08:32:30+00:00 )
Dec 24, 2023 08:32 UTC
  • Jeshi la Wanamaji la Iran lapokea makombora mapya ya cruise

Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limepokea mfumo wa kimkakati wa makombora ya cruis wa Talayieh na mfumo wa makombora wa Nasir na hali kadhalika helikopta za kwanza za vita vya kieletroniki na kijasusi.

Katika hafla iliyohudhuriwa na Admeri Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo Jumapili, mifumo hiyo mipya ya makombora imejumuishwa katika ukanda wa kusini wa manowari za jeshi hilo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, leo pia Jeshi la Wanamaji la Iran limepokea mifumo ya makombora ya ardhi kwa ardhi, ndege isiyo na rubani ya ‘Sanjar’ ambayo ina uwezo wa kumsaka adui na kisha kujilipua katika eneo lililoainishwa. Zana hizo mpya za kivita zinaweza kusehehniwa na meli ya kivita ya Jamaran.

Kombora la cruise la Talayieh lina uwezo wa kuruka masafa ya zaidi ya kilomita 1000 na ni kombora erevu ambalo linaweza kubadilisha eneo la kulenga shabaha kwa mujibu wa maelekezo na hivyo kumshtukiza adui.

Kombora la cruise la Nasir nalo lina uwezo wa kuruka masafa ya kilimota 100 na linatekeleza uharibifu mkubwa na sasa litatumika katika meli kadhaa za kivita..

Hali kadhalika mfumo wa vita vya kielektroniki uliowekwa katika helikopta za jeshi la majini unaweza kulinda meli za kivita za Iran na kuhadaa manowari za adui.

Zana hizo zote za kivita zilizozinduliwa leo zimeundwa nchini Iran kwa kutegemea utaalamu wa viwanda vya kijeshi nchini. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa uwezo wake wa kijeshi ni wa kujihami na una ujumbe wa amani kwa nchi jirani na rafiki na wakati huo huo ni onyo kwa maadui wenye nia mbaya dhidi ya nchi hii.