"Ubeberu wa US unaporomoka, muqawama ndiyo nguzo ya usalama katika eneo"
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Wamarekani wamekiri wenyewe kwamba, nidhamu ya dunia iliyojengeka katika misingi ya ubeberu ipo katika mkondo wa kuporomoka, na kwamba mabeberu hawawezi kuendelea kuwatwisha walimwengu misimamo na mitazamo yao.
Ali Baqeri Kani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la ISNA na kueleza kuwa, walimwengu wana uchu wa kuwa na nidhamu ya dunia yenye kuzingatia mantiki, iili iwe mbadala wa mfumo wa kibeberu wa Marekani.
Baqeri Kani amesema, katika zama za leo, Marekani katu haiwezi kuendelea kuibebesha dunia nidhamu ambayo msingi wake ni maslahi na matakwa ya Washington. "Vikosi vilivyopevuka vya muqawama katika eneo vina uwezo wa kufanya maamuzi huru katika kiwango cha kitaifa na kieneo," ameongeza afisa huyo wa ngazi ya juu wa Iran.
Amebainisha kuwa, jamii ya kimataifa inahitaji mfumo wa dunia ambao unatilia maanani maslahi ya mataifa huru duniani, na ambao utaleta amani na uthabiti katika kona zote za dunia.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza bayana kuwa, siasa za kibeberu za Marekani katika mahusiano ya kimataifa ndizo zinazohatarisha usalama wa dunia nzima na kukwamisha kupatikana utulivu wa kudumu.
Kani amesisitiza kuwa, Palestina itaendelea kuwa kadhia kuu ya umma wa Kiislamu, huku akitoa mwito kwa serikali za Kiislamu kuimarisha uungaji mkono wao kwa Wapalestina katika nyuga zote.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, kustawi kwa haraka fikra ya kuweko kambi kadhaa duniani ni ushahhidi kwamba mataifa ya dunia yameelewa kuwa mfumo wa kambi moja ni wa kidhalimu na si kitu cha kudumu.
Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amekosoa utendaji kazi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo linadai kwamba jukumu lake kuu ni kulinda na kudhamini amani na usalama wa dunia, akisisitiza kuwa, chombo hicho kimefeli, na ithibati ya hilo ni kushindwa kwake kuchukua hatua za maana za kukomesha mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.