Iran: Marekani haina ustahiki kuwatuhumu wengine; inachukiwa zaidi kwa kuiunga mkono Israel
-
Nasser Kan’ani
Iran imepuuzilia mbali shutuma "zisizo na thamani" za Marekani kwamba inazidisha mvutano katika bahari kuu, ikisema Washington, ambayo ni mshirika katika vita vya mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel kwenye Ukanda wa Gaza, "haina ustahiki" wa kutoa madai dhidi ya Tehran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan’ani, aliyasema hayo katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari siku ya Jumatatu, baada ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, kudai kuwa meli ya mafuta ya kemikali katika Bahari ya Hindi ilishambuliwa na ndege isiyo na rubani ya Iran.
Ameongeza kuwa Marekani inabeba jukumu la kuanza kwa vita vya Gaza mnamo Oktoba 7 na kuendelea kwake, na kuongeza kuwa, uungaji mkono wake kwa jinai za Israel umepelekea watu kote duniani waichukie.
Kan'ani amebaini kuwa: "Iran daima imekuwa ikihakikisha usalama katika bahari kuu, ilifanya kazi kwa uwajibikaji, na ilichukua jukumu muhimu katika usalama wa baharini. Kwa hiyo, Marekani na wengine hawapaswi kuishutumu Iran."
Katika mahojiano na gazeti la The Sunday Telegraph, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron pia alidai kwamba Iran "ni ushawishi mbaya kabisa katika eneo na ulimwengu."
Kan’ani amesema, Uingereza ambayo siku zote imekuwa na nafasi kubwa katika kuleta ukosefu wa uthabiti na ukosefu wa usalama katika eneo la Asia Magharibi, kisheria na kimaadili haifai kutoa shutuma dhidi ya Iran na nchi nyingine za eneo.
Amesema: "Uingereza yenyewe ni mshtakiwa wa vita vya Gaza, na bila shaka, nchi hiyo lazima iwajibike kwa hatua zake za zamani na za sasa kuhusu kuanzisha na kuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel kama kundi la kigaidi linalochukiwa zaidi katika eneo hilo."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amesema kuwa utawala wa Israel ulifanya "kosa la kimkakati" kwa kuchagua kuanzisha vita dhidi ya Gaza na kwamba umefanya "kosa kubwa zaidi la kimkakati" kwa kuendeleza uchokozi wake.