Sisitizo la Amir-Abdollahian la kutatuliwa matatizo kati ya Iran na Afghanistan
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya ulazima wa kutatuliwa masuala yaliyopo kati ya Iran na Afghanistan yakiwemo masuala ya mipaka na maji.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan. Katika mazungumzo yake na Amir Khan Muttaqi, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan, Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kubainisha matukio ya Gaza na mauaji ya kizazi yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda huo amesisitiza juu ya udharura wa kuweko ushirikiano wa mataifa yote ya Kiislamu na wapigania uhuru duniani katika kuwasaidia wananchi wa Palestina. Sanjari na hayo, Amir-Abdollahian alizungumzia pia uhusiano wa Iran na Afghanistan na kueleza matarajio aliyonayo kwamba, utawala wa sasa nchini Afghanistan utachukua hatua za haraka na za kivitendo kutatua matatizo yaliyopo baina ya pande mbili hizi.
Uhusiano wa Iran na Afghanistan katika wakati fulani umeshuhudia baadhi ya mvutano tangu Taliban waliposhika tena hatamu za uongozi wa nchi hiyo Agosti 2021, ambayo ni pamoja na suala la haki ya maji na mvutano wa mpaka.
Kutodhaminiwa haki ya maji ya Iran na kutokea ukame uliotokana na hilo ni jambo ambalo limewasababishia matatizo mengi wananchi wa Sistan na Baluchestan nchini Iran. Ni kwa msingi huo ndio maana, Iran inataka utekelezwaji makini na kamili wa vipengee vilivyoainishwa katika Mkataba wa 1351 kuhusu maji ya Helmand. Mto Helmand unatoka katika milima ya Hindu Kush ya Afghanistan kisha unatiririka hadi Iran, lakini Afghanistan imeathiri mtiririko wa maji yanayoingia Iran kwa kujenga kingo na mabwawa mbalimbali kwenye mto huo ili kukidhi mahitaji yake ya kilimo.

Ni dhahiri kwamba Taliban, kama kundi linalotawala hivi sasa nchini Afghanistan, limeahidi kutekeleza Mkataba wa Hirmand (Helmand) na kuipatia Iran haki yake ya maji kwa mujibu wa mkataba huo. Maafisa wa Taliban wametoa ahadi mara kadhaa kwamba, watashirikiana na maafisa wa Iran katika uwanja huu. Mfano wa wazi ni Amir Khan Muttaqi, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan ambaye huko nyuma amewahi kusisitiza kwamba, kundi hili linatambua rasmi haki ya maji ya Iran na kamwe halitaki kuisababishia Iran matatizo.
Matatizo kama vile magendo madawa ya kulevya, njama za makundi yenye silaha za kutaka kupenya na kuingia Iran kinyume cha sheria, na mapigano kadhaa kati ya vikosi vya Taliban na walinzi wa mpaka wa Iran pia yanachukuliwa kuwa miongoni mwa mambo ambayo yameathiri uhusiano kati ya Kabul na Tehran na hivyo kuzorotesha uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Hata hivyo pande zote mbili zimeweza kudhibiti mivutano hii na kuzuia kuongezeka na kushadidi kwa mzozo huo.
Pamoja na hayo, inapaswa kukumbwa kuwa, licha ya matatizo yaliyopo katika nyanja mbalimbali za kisiasa na kiusalama katika uhusiano kati ya Iran na Afghanistan, kama vile suala la haki ya maji ya Iran na masuala ya mipaka, lakini pande zote mbili zinatilia mkazo suala la kustawishwa kwa ushirikiano, hususan kuimarishwa mahusiano ya kibiashara na kiuchumi, jambo ambalo bila shaka, linaweza kuwa na taathira chanya katika kuhafifisha tofauti na mivutano katika nyuga zingine.
Afghanistan inapakana na Iran na inahesabiwa kuwa jirani muhimu kutokana na mambo yanayofanana kidini, kiutamaduni na kilugha na kuwepo kwa mpaka mrefu wa pamoja wa karibu kilomita 1000. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa haiachi kutoa msaada wowote kwa minajili ya kurejesha amani nchini Afghanistan na kutatua matatizo ya wananchi wa nchi wa nchi hiyo. Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, Iran imekuwa mwenyeji wa mamilioni ya wahajiri wa Kiafghani ambapo filihali kwa akali kuna wakimbizi milioni 5 wa Afghanistan wanaoishi nchini Iran ambapo wamekuwa wakinufaika na suhula zinazopatikana katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama raia wa Iran.

Katika hali hiyo, Taliban na serikali ya 13 ya Iran hivi sasa zimejikita katika kustawisha uhusiano ukiwemo uhusiano wa kiuchumi na safari za mara kwa mara za wajumbe wa nchi hizo mbili zinazojumuisha wataalamu na maafisa wa masuala ya uchumi, viwanda, biashara na kilimo zimekuwa zikifanyika katika fremu hiyo. Baraza la Wafanyabiashara wa Iran Novemba 6 mwaka huu lilikuwa mwenyeji wa ujumbe wa ngazi za juu wa Taliban, ambapo maafisa wa Afghanistan walionyesha nia yao ya kutumia uwezo wa sekta binafsi ya Iran.
Iran na Afghanistan pia zimetiliana saini mikataba mitano ya ushirikiano wa kiuchumi katika uga wa usafiri na uchukuzi, usafiri wa anga, madini na maeneo huria ya biashara. Mwezi Aprili mwaka huu Baraza la Wafanyabiashara na Uwekezaji la Taliban lilitangaza kuwa, kiwango cha biashara na Iran kimefikia dola bilioni moja kwa mwaka, na hivi sasa Iran ndiyo mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afghanistan.
Kwa muktadha huo, azma na matakwa ya viongozi ya Iran na Afghanistan ni kudumisha uhusiano na kuepuka ongezeko lolote la mvutano kati ya majirani hao wawili wa Kiislamu, na inatarajiwa, kama alivyosema Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran kwamba, kuchukuliwa hatua za kivitendo na Taliban na kutekelezwa hati za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili sambamba na kuongezwa mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi, kunapaswa pia kutatuliwa na kupatiwa ufumbuzi changamoto zilizopo katika nyanja za masuala ya maji na mipaka.