IRGC: Israel isubiri kisasi chetu kwa mauaji ya kamanda Sayyid Razi Mousavi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106492-irgc_israel_isubiri_kisasi_chetu_kwa_mauaji_ya_kamanda_sayyid_razi_mousavi
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema Iran itatoa jibu ipasavyo kwa utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya mauaji ya mshauri mkuu wa kijeshi wa IRGC nchini Syria, na ameahidi kulipiza kisasi kwa shambulio hilo la kigaidi katika nyakati na maeneo tofauti.
(last modified 2023-12-27T10:56:53+00:00 )
Dec 27, 2023 10:56 UTC
  • Ramezan Sharif
    Ramezan Sharif

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema Iran itatoa jibu ipasavyo kwa utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya mauaji ya mshauri mkuu wa kijeshi wa IRGC nchini Syria, na ameahidi kulipiza kisasi kwa shambulio hilo la kigaidi katika nyakati na maeneo tofauti.

Brigedia Jenerali Ramezan Sharif aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari leo Jumatano, baada ya kamanda wa IRGC, Sayyad Razi Mousavi kuuawa katika shambulio la anga la Israel katika kitongoji cha Sayyida Zainab katika mji mkuu wa Syria, Damascus.

Amebainisha kuwa, mauaji ya Mousavi ni mwendelezo wa ukiukaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel na kuitaka jamii ya kimataifa kusimamisha jinai za utawala huo katili zinazohatarisha amani na usalama wa kimataifa.

Sayyid Razi Mousavi, ambaye alikuwa mshauri wa kijeshi nchini Syria, aliuawa katika shambulizi la anga la Israel katika kitongoji cha Sayyida Zainab katika mji mkuu wa Syria, Damascus mapema jana Jumatatu.

Sayyid Razi Mousavi, alikuwa mmoja wa masahiba wa kamanda mkuu wa Iran wa kupambana na ugaidi, Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Awali, Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, alisema utawala wa Kizayuni wa Israel utalipa gharama ya kitendo chake cha uhalifu cha kumuua mshauri mkuu wa kijeshi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) nchini Syria.

Katika ujumbe wake uliotolewa Jumatatu iliyopita, Sayyid Ebrahim Raisi alisema kitendo kiovu cha kumuua kigaidi mshauri wa jeshi la IRGC katika shambulio la makombora nchini Syria ni ishara nyingine ya kukata tamaa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Iran imetuma ujumbe wa washauri nchini Syria kwa ombi la serikali ya Damascus kwa lengo la kusaidia nchi hiyo ya Kiarabu iliyoharibiwa na vita kupambana na wanamgambo wanaoungwa mkono na mataifa ya kigeni ambao wamekuwa wakipigana na serikali ya Syria iliyochaguliwa kidemokrasia tangu 2011.