Lavrov: Russia inaheshimu bila masharti mamlaka ya ardhi yote ya Iran
Sergei Lavrov Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amesema kuwa, Russia inaheshimu kwa dhati na kiukwelii kabisa tena bila masharti mamlaka ya ardhi yote ya ardhi ya Iran na kwamba, huu ni msimamo usiobadilika wa Moscow.
Lavrov amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na kusisitiza kwamba, taifa hilo linaheshimu kikamilifu mamlaka ya ardhi yote ya Iran.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia ametangaza msimamo huo siku chache baada ya nchi hiyo kuunga mkono madai ya Imarati kuhusu visiwa vitatu vya Iran.
Mkutano wa Sita wa Baraza la Ushirikiano la Nchi za Kiarabu na Russia ulifanyika tarehe 20 mwezi huu wa Disemba mwenyeji akiwa ni Nasser Burita Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco; na kwa mara nyingine tena katika taarifa ya mwisho ya mkutano huo Imarati ikatoa madai kuhusu visiwa vitatu vya Iran, yaliyoungwa mkono na Russia.

Katika miaka ya karibuni Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) umetoa madai mara kadhaa ya ardhi kuhusu visiwa hivyo vitatu vinavyomilikiwa na Iran.
Msimamo wa Russia wa kuunga mkono madai ya Imarati ulikosolewa pakubwa na fikra za waliowengi na baadhi ya viongozi na shakhsia mbalimbali wa Iran ambao wameutaja kuwa unakinzana na mchakato unaopiga hatua wa uhusiano kati ya Tehran na Moscow.