Mwandishi habari: Palestina itakuwa huru iwapo Waislamu wote wataisaidia kama inavyofanya Iran
Mwandishi wa habari kutoka Ukanda wa Gaza amepongeza uungaji mkono usioyumba wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina kwa miongo kadhaa sasa na kuongeza kwamba, ardhi za Palestina zingekombolewa kutoka mikononi mwa ukoloni na uvamizi wa Israel ikiwa serikali zote za Kiislamu zingesaidia Wapalestina kama Iran inavyofanya.
Israa Al-Buhaisi, ambaye sasa ni mwandishi wa Televisheni ya Al-Alam ya lugha ya Kiarabu ya Iran, aliyasema hayo katika ujumbe wa video uliorushwa katika mkutano wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei na makundi ya wanawake mjini Tehran siku ya Jumatano.
Amesema katika hotuba yake: "Nyinyi, taifa la Iran, ndio taifa pekee ambalo limekuwa likisimama pamoja na Palestina na Msikiti wa al-Aqsa. Iran imelengwa kwa vikwazo vikali zaidi na mashinikizo kutokana na msaada wake kwa Palestina"
Aidha amesema: "Nawaombeni msiwaache peke yao watu wa Palestina na Gaza na mjue kwamba Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi."
Gaza imekuwa ikikabiliwa na vita vya maangamizi ya umati kutoka kwa utawala haramu wa Israel tangu Oktoba 7.
Vita hivyo vya umwagaji damu mkubwa zaidi kuwahi kutokea huko Gaza hadi sasa vimeua zaidi ya Wapalestina 21,000, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, na kujeruhi wengine zaidi ya 55,000, huku maelfu ya wengine wakiaminika kupotea na kufukiwa chini ya vifusi. Utawala dhalimu wa Israel pia umekata maji chakula na usambazaji umeme huko Gaza.
"Al-Buhaisi katika ujumbe wake amesema: "Endeleeni kuwaunga mkono watu wa Palestina kama ambavyo mumekuwa mkifanya hadi sasa. Kama msimamo na uthabiti wa nchi zote za Kiislamu ungekuwa kama Iran, bila shaka ardhi ya Palestina ingekombolewa kufikia sasa"
Iran ilianza kuwaunga mkono Wapalestina mara tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, huku marehemu mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Khomeini, akiielezea Israel kama "uvimbe wa saratani" ambao lazima uondolewe katika eneo.
Kwa muda mrefu Iran imependekeza kura ya maoni kwa kuwashirikisha wakaazi wote wa asili wa ardhi ya Palestina na vizazi vyao kama suluhuhisho la kudumu la mzozo wa muda mrefu huko Palestina.
Iran pia imeziunga mkono harakati za kupigania ukombozi wa Palestina katika mapambano ya kurejesha haki za taifa hilo linalodhulumiwa.