Iran yataka E3, Marekani kuacha mashinikizo dhidi ya mpango wake wa nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106588-iran_yataka_e3_marekani_kuacha_mashinikizo_dhidi_ya_mpango_wake_wa_nyuklia
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Marekani lazima ziache kutoa matamshi na mashinikizo yasiyo na matunda dhidi ya Tehran na badala yake zichukue hatua zinazohitajika za kisiasa.
(last modified 2023-12-30T04:22:22+00:00 )
Dec 30, 2023 04:22 UTC
  • Iran yataka E3, Marekani kuacha mashinikizo dhidi ya mpango wake wa nyuklia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Marekani lazima ziache kutoa matamshi na mashinikizo yasiyo na matunda dhidi ya Tehran na badala yake zichukue hatua zinazohitajika za kisiasa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani alitoa kauli hiyo Ijumaa akijibu taarifa ya pamoja iliyotolewa Alhamisi na pande tatu za Ulaya na Marekani kuhusu makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja wa JCPOA.

Taarifa ya nchi za Magharibi imelaani kile kinachodaiwa kuwa ni hatua ya Iran ya kuongeza kiwango cha uzalishaji wa madini ya urani yaliyorutubishwa hadi kiwango cha asilimia 60.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesisitiza kuwa mpango wa nyuklia wa Iran unafuatilia malengo ya amani pekee. Amesema Tehran bado inaamini kuwa diplomasia ndiyo njia bora zaidi ya kuondoa wasiwasi usio na msingi kuhusu shughuli za amani za nyuklia za Iran.

Kan’ani amesema kuwa: “Sasa mpira uko kwenye uwanja wa Marekani na nchi tatu za Ulaya. Wanapaswa kuchukua maamuzi muhimu ya kisiasa kwa kuachana na sera ya kutoa kauli na mashinikizo yasiyo na matunda."

Aidha amekumbusha kuwa, Marekani na nchi tatu za Ulaya zinazojulikana kama E3 zilijiondoa kwenye meza ya mazungumzo na kwa hivyo hazina ustahiki wa kutoa maoni yoyote kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa: "Urutubishaji katika kiwango cha asilimia 60 katika vituo vya kurutubisha urani daima umekuwepo na utaendelea kwa mujibu wa mahitaji ya amani ya nchi na chini ya usimamizi kamili wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Kan’ani amesema badala ya kufuata sera ya kulaumiana na kuchukua misimamo inayochochewa kisiasa, Marekani Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zinapaswa kutathmini vyema utendaji wao kuhusu mazungumzo ya kuondoa vikwazo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kuangalia matokeo ya sera zao zisizo na manufaa.

Msemaji huyo amesisitiza msimamo wa Iran katika kuendeleza ushirikiano na IAEA.

Hali kadhalika Kan'ani amesisitiza kuwa, madai ya upande mmoja na kutokuwa tayari kurekebisha hatua mbaya zilizochukuliwa na nchi za Magharibi hazitasaidia kutatua suala la nyuklia.

Mwezi Mei 2019, mwaka mmoja baada ya Marekani kuchukua hatua ya upande mmoja ya kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Iran ilianza kuchukua hatua za kupunguza ahadi zake chini ya makubaliano hayo baada ya Umoja wa Ulaya kushindwa kutimiza ahadi zake.

Tehran ilianza hatua kwa hatua kuondoa kizuizi kilichowekwa katika JCPOA juu ya shughuli zake za nyuklia. Wakati huo, Iran  ilisisitiza kuwa kama uchumi wake ungelindwa dhidi ya vikwazo, ingebadilisha uamuzi wake wa nyuklia.