Iran yakosoa taarifa ya Arab League, yasema itaendelea kuwaadhibu watenda jinai
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali taarifa ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu hatua ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ya kufanya shambulio la makombora dhidi ya kituo kikuu cha ujasusi cha shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mossad katika eneo la Kurdistan ya Iraq.
Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema katika taarifa leo Ijumaa kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasita kuendelea kuwaadhibu na kuwatia adabu watenda jinai wanaohatarisha usalama wa nchi hii.
Amesema Arab League inapasa kuelekeza nguvu na jitihada zake za kisiasa, kiusalama na kisheria dhidi ya utawala katili wa Israel ambao unaendelea kufanya mashambulizi ya maangamizi ya kizazi katika Ukanda wa Gaza.
"Arab League inatarajiwa ifanye juhudi za kusimamisha ukaliaji wa mabavu wa miaka 75 wa ardhi za Palestina, na iliunge mkono taifa madhulumu la Palestina," ameongeza Kan'ani.
Ameeleza bayana kuwa, mashambulizi yaliyofanywa na IRGC dhidi ya ngome za magaidi nchini Syria na kituo cha ujasusi cha utawala wa Israel nchini Iraq ni sehemu ya "adhabu ya haki" dhidi ya wanaokiuka usalama wa Iran baada ya shambulio baya la kigaidi katika mji wa Kerman.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, "Hatua hiyo ilikuwa ya kutetea mamlaka na usalama wa nchi, na kukabiliana na ugaidi, na ni sehemu ya adhabu ya haki ya Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya wanaokiuka usalama wa nchi."
IRGC ilitangaza kuwa, shambulio lake la makombora katika eneo la Kurdistan ya Iraq lililenga na kukiangamiza kikamilifu kituo cha kijasusi cha Mossad katika eneo hilo. Jeshi la SEPAH lilifafanua kuwa, kituo hicho cha Mossad kilitumika "kuendeleza operesheni za kijasusi na kupanga vitendo vya kigaidi" katika eneo zima, hususan nchini Iran.
Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, Tehran haitasita kutumia haki yake halali na ya kisheria ili kuzuia vyanzo vyote vya vitisho dhidi ya usalama wa taifa lake, kutetea raia wake na kuwaadhibu wahalifu.