Jan 20, 2024 03:00 UTC
  • Azma thabiti ya Iran na Pakistan ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kupambana na ugaidi

Baada ya kushadidi mivutano ya mpakani kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan katika kipindi cha siku mbili zilizopita, viongozi wa Tehran na Islamabad wamesisitiza kuendeleza uhusiano wa kirafiki kati ya nchi mbili, kuheshimiwa umoja wa ardhi za mataifa hayo mawili na kuwepo uratibu na mashauriano ya karibu zaidi katika kupambana na magenge ya kigaidi.

Katika matamshi aliyotoa siku ya Alkhamisi kuhusiana na operesheni zilizotekelezwa Jumatano na Alkhamisi kwenye pande mbili za mipaka ya Pakistan na Iran, Rais Arif Alvi wa Pakistan alisema, Islamabad ina uhusiano wa muda mrefu na wa kindugu na Tehran, kwa hivyo zinachopaswa kufanya nchi hizo mbili ni kutumia njia za kidiplomasia katika kutatua masuala mbalimbali ikiwemo hatari ya ugaidi na kukosekana kwa usalama wa mipakani.

Rais Arif Alvi wa Pakistan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian alisema katika mazungumzo ya simu aliyofanya na mwenzake wa Pakistan, Jalil Abbas Jilani, kwamba usalama wa Pakistan ni usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akabainisha kuwa, genge la kigaidi linalojiita Jaishul-Adl, ambalo linajulikana nchini Iran kama Jaishul-Dhulm ni kundi la kigaidi linalofanya vitendo vinavyohatarisha usalama wa nchi zote mbili.

Akizungumzia kushambuliwa kwa maficho ya kundi moja la magaidi wa Jaishu-Dhulm kwenye ukanda wa mpaka wa Pakistan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema, usalama wa Iran umekuwa ukihatarishwa mara kwa mara na kundi hilo la kigaidi kutokea kwenye ardhi ya Pakistan; na harakati zinazoongezeka kila uchao za kundi hilo, ndizo zilizopelekea Iran kufanya shambulio siku ya Jumatano lililolenga makao yake yaliyoko ndani ya ardhi ya Pakistan.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian

Katika mazungumzo hayo ya simu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan aliashiria malengo makuu ya pamoja ya nchi mbili na historia ya Iran na Pakistan katika kuteteana na kupambana na ugaidi na akasisitiza kwa kusema, usalama wa Iran ni usalama wa Pakistan na kila kinapotokea kitisho ndani ya ardhi ya nchi hiyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, serikali ya Islamabad imechukua hatua ya kukabiliana nacho.

Pamoja na hayo, Jilani alisema Islamabad inaitakidi kuwa kukabiliana na magenge ya kigaidi ndani ya nchi hizo mbili inapasa kufanywe zaidi kwa uratibu pande mbili na kwa kutumia vikosi vya ndani ya nchi husika.

Siku ya Jumatano, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilishambulia makao ya kundi la kigaidi la Jaishu-Dhulm karibu na mpaka wa Pakistan, ikikumbukwa kuwa, wiki mbili zilizopita, mji wa Kerman ulioko kusini mwa Iran ulishuhudia shambulio la kigaidi la umwagaji mkubwa wa damu lililolenga watu waliokuwa wakielekea kwenye hauli ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qasem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Watu wanaokaribia 100 waliuawa shahidi katika shambulio hilo. 

Mbali na shambulio hilo la kigaidi la mkoani Kerman, Desemba 15, 2023 , eneo la Rask la mkoa wa Sistan na Baluchistan, lililoko karibu na mpaka wa Pakistan, lilishuhudia kwa mara nyingine shambulio la kigaidi, ambapo askari 11 wa jeshi la Polisi waliuawa shahidi kwenye hujuma hiyo iliyolenga makao ya polisi ya eneo hilo.

Operesheni ya IRGC dhidi ya ngome za magaidi

Baada ya mashambulizi hayo ya kigaidi, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilitekeleza operesheni za mashambulio kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani zilizolenga ngome za magaidi katika eneo la Arbil nchini Iraq na ndani ya ardhi za Syria na Pakistan.

Operesheni hizo zilitekelezwa baada ya maonyo kadhaa yaliyotolewa na Iran kwa wanaowaunga mkono magaidi wa eneo hili; na licha ya juhudi za vyombo vya habari vya Magharibi na vya Kizayuni za kuishutumu Iran, wataalamu na maafisa wa kisiasa wa nchi mbalimbali waliitaja hatua hiyo ya Iran kuwa ni haki ya kulinda umoja wa ardhi yake.

Mkabala na operesheni zilizotekelezwa na Iran, siku ya Alkhamisi asubuhi, Pakistan ilikishambulia kijiji cha mpakani ndani ya ardhi ya Iran karibu na Saravan katika mkoa wa Sistan na Baluchistan, ikidai kwamba shambulio hilo lililoua watu tisa lililenga kuteketeza maficho ya kundi la kigaidi linalojulikana kama Sarmchar.

Shambulio hilo ambalo lilifanywa bila mashauriano yoyote na Iran, lilishuhudiwa katika hali ambayo, huko nyuma serikali tofauti za Pakistan zilishasisitiza mara kadhaa juu ya haja ya kupanuliwa ushirikiano wa pande mbili, hususan katika nyanja za kibiashara, kiuchumi na kiusalama.

Wakati viongozi wa Pakistan wanasisitiza kuimarishwa uhusiano wa kirafiki hasa katika uga wa uchumi, sharti la kwanza na muhimu zaidi la kustawisha mabadilishano ya kiuchumi na kibiashara katika mpaka wa nchi mbili wenye urefu wa kilomita 900 ni kuhakikisha amani na utulivu vinatawala katika eneo hilo; lakini kuwepo kwa harakati za magenge ya kigaidi kama vile kundi lijiitalo Jaishul-Adl katika maeneo ya mipakani ni kizuizi cha kufikiwa lengo hilo.

Kwa mtazamo wa Iran, licha ya kufanyika vikao na mazungumzo mengi ya pamoja kati ya maafisa wa mipaka, usalama, jeshi na polisi wa Iran na Pakistan na makubaliano mengi yaliyofikiwa juu ya kufanyika juhudi za pamoja za pande mbili husika kwa ajili ya kuimarisha usalama wa mipaka na kushirikiana katika mapambano dhidi ya ugaidi, upande wa Pakistan haujalitekeleza jukumu hilo kama inavyostahiki.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba miaka michache iliyopita, serikali ya Pakistan ilitoa orodha ya makundi ya kigaidi yaliyoko nchini humo, yakiwemo makundi 74 ya wabeba silaha, mengi yao yakiwa katika mkoa wa Baluchistan wa nchi hiyo na jirani na mpaka wa Iran; ukiwa ni ushahidi tosha wa hali hatari ya kiusalama inayotawala ndani ya nchi hiyo na katika eneo.

Kwa upande mwingine, kwa kuzingatia uwezo wa jeshi na vikosi vya usalama vya Pakistan, haionekani kuwa ni kazi ngumu kwa Islamabad kudhamini usalama wa maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Iran na kuyasafisha maeneo hayo ili kusiwepo na magenge ya kigaidi likiwemo la Jaishul-Adl na hasa kwa vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imeishaitaarifu Pakistan mara kadhaa kuhusu utayari wake wa kushirikiana nayo bega kwa bega katika kupambana na magaidi na majambazi kwenye maeneo ya mpakani.

Sambamba na hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza mara kadhaa kuwa haina mzaha na mtu yeyote katika suala la kudhaminiwa usalama wake; na ni wazi kwamba takwa dogo zaidi la wananchi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa jirani yake wa mpaka wa mashariki ni kupewa uzito mkubwa zaidi usalama wa mipaka na kuchukuliwa hatua athirifu za kupambana na magaidi katika maeneo ya mpakani. Kwa hiyo kuimarishwa usalama ni sharti la kawanza na muhimu zaidi kwa ustawi wa shughuli za kiuchumi na miamala ya kibiashara katika mpaka mrefu wa pamoja wa Iran na Pakistan yakiwemo magulio ya mpakani…/

 

Tags