Pakistan yatangaza kurejesha uhusiano kamili na Iran baada ya mivutano iliyojitokeza
(last modified Sat, 20 Jan 2024 06:53:04 GMT )
Jan 20, 2024 06:53 UTC
  • Pakistan yatangaza kurejesha uhusiano kamili na Iran baada ya mivutano iliyojitokeza

Pakistan imetangaza kurejesha kikamilifu uhusiano wa kidiplomasia na Iran baada ya kujitokeza mivutano mikali ya mpakani ambayo haijawahi kushuhudiwa kati ya nchi mbili juu ya operesheni za kupambana na ugaidi.

Tangazo hilo lilitolewa jana Ijumaa baada ya Waziri Mkuu wa muda wa Pakistan Anwar-ul-Haq Kakar kufanya mkutano wa dharura wa usalama na wakuu wa kijeshi na wa kiintelijensia kujadili hali ya taharuki iliyojitokeza hivi majuzi.
 
Vyombo vya habari vya Pakistan vimeripoti kuwa Islamabad imekubali kurejesha uhusiano kamili wa kidiplomasia na Iran na kwamba mabalozi wa Iran na Pakistan karibuni hivi watarejeshwa kwenye vituo vyao vya kazi.
 
Kakar alieleza hapo jana kwamba ni kwa manufaa ya Iran na Pakistan kuchukua hatua ya kurejesha uhusiano wao katika ngazi ya kabla ya mvutano uliozuka hivi majuzi.
 
Waziri Mkuu wa muda wa Pakistan alisema "ni kwa manufaa ya nchi zote mbili kuchukua hatua ya kurejesha uhusiano kama ulivyokuwa kabla ya Januari 16."
 
Kakar ameongezea kwa kusema, Pakistan "itakaribisha na kufuatiza hatua zote chanya zitakazochukuliwa na upande wa Iran" juu ya suala hilo.
Kikao cha Baraza la Mawaziri la Pakistan

Amesema Pakistan na Iran ni "nchi mbili ndugu ambazo kihistoria zimekuwa na uhusiano wa kiudugu na ushirikiano uliotawaliwa na heshima na upendo."

 
Kakar ameongeza kuwa, Pakistan ni "nchi inayotii sheria na kupenda amani", inayotaka kuwa na uhusiano wa kirafiki na ushirikiano na nchi zote, hasa majirani zake.

Mapema jana hiyohiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Jalil Abbas Jilani na mwenzake wa Iran Hossein Amir-Abdollahian walifanya mazungumzo kwa njia ya simu na kutoa wito wa kuwepo ushirikiano wa karibu katika nyanja mbalimbali ikiwemo kupambana na ugaidi na kuimarisha usalama mipakani.

"Jilani alionyesha utayari wa Pakistan kufanya kazi na Iran katika masuala yote kwa msingi wa moyo wa kuaminiana na kushirikiana," ilieleza taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan na kuongeza kuwa mwanadiplomasia huyo mkuu wa Islamabad "alisisitiza haja ya kuwepo ushirikiano wa karibu katika masuala ya usalama".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran naye pia alisema katika taarifa yake kwamba, mamlaka na umoja wa ardhi ya Pakistan ni jambo linalopewa umuhimu mkubwa na Iran na ni muhimu kwa nchi hizo mbili kushirikiana katika kuzima hujuma na kutokomeza kambi za magaidi zilizoko Pakistan.

Akiashiria operesheni ya hivi majuzi ya Iran dhidi ya kundi la kigaidi la Jaishul-Adl nchini Pakistan, Amir-Abdollahian alisema, operesheni hiyo ilifanywa ili kuzima tishio la shambulio la kigaidi lililokuwa likikaribia kutekelezwa.../

 

Tags